Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

YAJUE MAMBO HAYA 10 YANAYOMTAMBULISHA MWANAMKE MPENDA PESAKATIKA zama hizi kuliko zama zingine zozote pesa imepewa kipaumbele kikubwa katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi. Mwanamke asiyempenda mtu bali pesa si rahisi kujenga uhusiano wowote wa maana na mwanamume maskini, au yule ambaye hatakuwa na uwezo wa kutimiza mahitaji yake makubwa. Hata kama una pesa, ni gharama sana kumfanya mwanamke mpenda pesa kuwa na furaha. Naam, yupo mwanamke ambaye hataki mapenzi wala chochote kwa mwanamume bali faida ya fedha au mali . Huyu hawezi kufurahishwa kwa chochote kile pungufu ya matakwa yake ya fedha na mali . Katika pitapita zako unaweza kuukwaa mkenge na kujikuta umeingia katika uhusiano na mwanamke wa aina hii, au ukajikuta ukimfukuzia mwanamke huyu ambaye hampendi mtu bali pesa. Unapaswa kuwa mjanja na kumbaini mwanamke huyu kabla hajakupotezea muda na kukuingiza hasara. Yafuatayo ni mambo 10 ambayo yatakuonesha kuwa mwanamke uliye naye au unayemfuatilia hakupendi bali anapenda waleti yako: - 1. ANAPENDA ZAWADI ZA BEI MBAYA Mwanamke anayependa pesa, unapompa kitu, hata kama ni kizuri lakini kikawa ni cha bei rahisi, hata kama kitu hicho ni kumbukumbu muhimu ya jambo fulani maisha mwenu hatakithaimini, kwani atafikiria tu gharama yake, maana yeye ni mtu wa gharama. Pia, si rahisi kumfurahisha mwanamke huyu kwa mashairi ya kimapenzi. Yeye anachokitaka kwako ni pesa, kwani mistari hailiwi. Kwake yeye mikono mitupu hailambwi. Utakapompa zawadi unayoidhania kuwa ya kiubunifu, yeye moyoni mwake atakuwa anatamani ungempa hereni za dhahabu au viatu vya kisasa alivyowahi kukutajia kuwa anavitaka. Mwanamke huyu hapendi zawadi tu ilimradi, bali zawadi ambazo hata watu watakaomwona nazo wajue ni mtu wa bei mbaya. Yeye masuala ya kumbukumbu na hisia hayamhusu. 2. MARAFIKI ZAKE NI WAPENDA PESA Watu husema ni rahisi kubaini tabia ya mtu kwa kuwaangalia wale anaoambatana nao. Iwapo utabaini kuwa mpenzi wako au mwanamke unayemfukuzia muda wake mwingi huutumia na wanawake wanaoonesha kila dalili kuwa ni wa aina ya “hapendwi mtu”, au pengine umesikia tetesi kuhusiana na mwenendo wa wanawake hao, basi kuna kila dalili kuwa mpenzi wako huyu ameshaathiriwa nao, au anaambatana nao kwa sababu wana tabia sawa. Katika hali hii, kuwa makini na usiondoe mkono wako ilipo waleti yako. Hatakuibia, lakini kwa hakika ni mtu wa kupenda pesa, matanuzi na vitu vya bei mbaya. 3. ATATAKA SANA KUJUA MAISHA YAKO Unaweza kubaini kuwa msichana uliyekutana naye ana hamu sana ya kufahamu kuhusiana na kazi yako na kipato chako tangu siku ya kwanza ya kukutana naye. Unaweza kupotea, ukadhani pengine amekupenda sana na anataka kufahamu maisha yako ili aweze kukupenda kwa dhati na uhakika zaidi. Lakini ukweli mwingine unaweza kuwa kwamba mwanamke huyu anataka kujihakikishia kama una uwezo wa kukabiliana na mahitaji yake makubwa, maana kwa hakika ni mtu anayependa maisha ya hali ya juu. 4. HATAGHARIMIA CHOCHOTE, POPOTE Ukiwa na mwanamke mpenda pesa, siku zote bili inapotokea pengine mmekaa mahala mnakula na kunywa atajifanya kama vile haioni. Ni kweli kuwa kawaida wanaume ndio hulipa, pengine kutokana na ukweli kwamba ndio wenye jukumu kubwa katika kuanzisha uhusiano, lakini kama mwanamke anafanya kazi anapaswa angalau kuonesha nia ya kusaidia. Kwa mwanamke huyu mpenda pesa, malipo yote ni juu yako, hutatarajia kuwa atalipa au kutaka mchangie gharama. Mwanamke huyu atachukulia tu kuwa wewe ni muungwana na huwezi kumdai. Utakapoonekana kutosita kulipa, utajipatia “mapenzi” makubwa kutoka kwa mwanamke huyu. 5. ANAWACHUKIA WANAWAKE WENZAKE Mwanamke mpenda pesa mara zote atakuwa amevaa mavazi ya kifahari pamoja na mapambo mbalimbali. Kwa hakika, huyu ni mwanamke anayejijali sana kwa kila analoweza japo ni kwa kutumia pesa za wanaume. Kwa kuwa mwanamke huyu ataweka mkazo zaidi katika mwonekano wake, atakuwa mtu wa wasiwasi kuhusiana na wanawake wenzake na pia atakuwa na mashindano, hususan wanawake wale anaodhani wanaweza kuwa tishio kwake sokoni. Mwanamke huyu ataepuka sana kuwa katika kampani moja na wanawake wanaoweza kuwa washindani wake. Naam, maisha yake yatakuwa ya kutokujiamini katika eneo hili. 6. HUTUMIA UREMBO WAKE KAMA TANZI Mwanamke mpenda pesa, akiwa pia amejaliwa uzuri wa sura na maumbile ni rahisi sana kuyatumia majaliwa yake haya kwa manufaa ya muda mfupi. Mwanamke huyu anaweza kuwa na tabia za kichangudoa, mathalani kukaa “vibaya” au kuonesha makusudi baadhi ya maeneo muhimu ya mwili, mathalani kitovu, kwa lengo la kumvutia mwanamume kwa maslahi yake ya kifedha. Wakati mwingine mwanamke huyu anaweza kuwa ana shida, pengine tairi la gari lake limepata mushkili na anataka msaada wa mtu kumbadilishia, atamwendea katika hali ya kumtamanisha ili aweze kumsaidia katika tatizo hili. Yawezekana hata wewe unayemfuatilia au uliye naye sasa alikupata kwa njia kama hii. Hata hivyo, yamkini malengo yake si ya muda mrefu, kwani anachokitaka kwako ni pesa na mali tu. 7. HUPENDA SANA KUONEKANA WA HADHI YA JUU Ni jambo la kawaida kwa mwanamke mpenda pesa pia kupenda kuonekana wa “matawi ya juu”. Mara nyingi, mwanamke huyu atadhani kuwa atapata hadhi hiyo kwa kutegemea na jinsi anavyoonekana, hususan mavazi, mtindo wa nywele zake na mapambo yake mwilini. Mwanamke huyu ana tabia ya kuwapuuza na kuwabeza watu ambao anadhani hadhi yao ni ya chini – mathalani watu wasio na nyumba, magari, wenye kazi za hadhi ya chini na kadhalika. Anapotoka na mwanamume atafurahi sana iwapo mwanamume huyo atamwambia anamiliki gari la kifahari kama vile Benz na Lexus, badala ya magari ya kawaida ambayo kila mtu analo. 8. HUWATUMIA WANAUME KAMA NGAZI Mwanamke mpenda pesa mara nyingi huwatumia wanaume kama ngazi zake za kupandia katika nyanja mbalimbali za kimaisha kama vile kazini, kwenye biashara, shuleni na kwingineko. Na mara nyingi baada ya kupata kile alichokipata, atambwaga mwanamume anayehusika na ikibidi kumtafuta mwingine ambaye mambo yake ni makubwa zaidi. Iwapo utafanikiwa kuipata historia ya mwanamke huyu utabaini kuwa ana wanaume wengi ambao amewahi kuwa nao. Ukichunguza zaidi, utabaini kuwa alikuwa akiwabwaga mmoja baada ya mwingine kwa kuzingatia hadhi na ukwasi, si mapenzi. Yamkini nawe kuna kitu amekupendea ambacho wale aliokuwa nao zamani hawakuwa nacho, ilimradi tu ni kitu chenye manufaa kwake kifedha au kimaisha. 9. MWONEKANO WAKE SI SAIZI YAKO Unapokuwa na mwanamke ambaye watu wote wanaomfahamu wanakubaliana na ukweli kuwa ni mrembo na hususan wanaume wengi wanamwogopa kwa urembo wake, lazima utajisikia vema na utajiamini zaidi kuwa na wewe ni babu-kubwa. Lakini utajisikia vizuri zaidi kama hujioni kustahili kuwa naye, pengine wewe mwonekano wako ni wa kawaida na hujawahi kuitwa “handsome” hata kwa kutaniwa. Hata hivyo, zali lako hili linaweza kuwa ishara mbaya kwa upande wa aina ya mwanamke uliye naye. Mwanamke mpenda pesa anaweza kuingia katika uhusiano na mwanamume yeyote, akiwemo yule ambaye kila mtu atasema hamstahili, ilimradi pesa iwepo na mahitaji yake yote ya bei mbaya yaweze kutimizwa. Usishangae basi kuwa mwanamke huyu amekuja kuchuna buzi tu na ikitokea mambo yako yakawa hayaendi vizuri atakubwaga tu kisha kukuona kama ganda la muwa la jana. 10. HUJIONA MWENYE KUSTAHILI KILA JEMA Mwanamke mpenda pesa na mali mara nyingi hatakuwa na malengo ya muda mrefu katika uhusiano na mtu. Ni kweli wanawake hawa hufikia wakati wakaolewa, lakini mara nyingi wakati wa ujana wao hawana malengo yoyote ya kudumu na mwanamume. Kisakolojia, hali hii humfanya kujihisi kama vile kila anachokipata kwa mwanamume ni stahili yake. Mwanamke huyu hujihisi kustahiki kupata maisha mazuri, kupata vitu vya thamani kubwa, kupata kazi, kupanda cheo kazini na kadhalika bila kulazimika kuinua mkono wake uliojazwa dhahabu kufanya kazi kama wanawake wengine. JIEPUSHE NAYE Hakuna mwanamume ambaye kwa makusudi kabisa atataka kuingia katika uhusiano na mwanamke ambaye malengo yake ni kuchuna buzi tu na kuondoka zake. Ni kweli kuwa wapo wanaume wanaolipia mapenzi, mathalani kwa makahaba, lakini angalau mtu anayefanya hivi anajua uhusiano huu ni wa dakika chache na hakuna mapenzi yoyote bali ngono. Ukiisha kuzifahamu ishara hizi muhimu za mwanamke mpenda pesa na mali , unaweza kujiepusha naye, usije ukaishia kujuta maisha yako yote huku ukiwa umeshapoteza muda wako na mali nyingi, nyumba umeshamjengea na magari umemnunulia. Kumbuka majuto ni mjukuu. Ushauri: 0654 043953

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top