SERIKALI imetangaza kuwachukulia hatua kali waajiri mbalimbali wanaokiuka sheria za usalama wa mfanyakazi mahali pa kazi na hivyo kuhatarisha maisha ya wafanyakazi, anaandika Dany Tibason.
Anthony Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu ameyasema hayo mbele ya watumishi wa wakala wa usalama na afya mahali pa kazi (OSHA) pamoja na waandishi wa habari katika maashimisho ya miaka 15 ya kuanzishwa kwa OSHA.
“Waajiri wote wanatakiwa kuzingatia Sheria ya usalama wa wafanyakazi mahali pa kazi, na mwajiri atakayeonekana kuwafanyisha kazi wafanyakazi wake bila kuchukua tahadhari za kuwakinga kiusalama atachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesma Mavunde.
Mavunde amewataka wafanyakazi, kutoa taarifa serikalini pale wanapoona mambo hayaendi vyema, ili hatua za sheria zichukuliwe kwa waajiri wanaoenda kinyume na utaratibubu na kwamba hatua zitachukuliwa bila kujali ni taasisi gani imekiuka sheria.
Naye Dk. Akwelina Kayumba, mtendaji mkuu wa OSHA, amesema moja kati ya changamoto kubwa zinazowakabili wafanyakazi ni waajiri wengi kutowapatia vitendea kazi wafanyakazi wao wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.
“Tunatoa elimu kwa jamii na waajiri wa kada mbalimbali ili wajue umuhimu wa kuwapatia vifaa watumishi wao, na katika maadhimisho ya kutimiza miaka 15 ya OSHA, tutafanya usafi katika maeneo ya Stendi ya Mabasi yaendayo mikoani pamoja na maeneo mengine ya Manispaa ya Dodoma,” amesema.
Post a Comment