SAKATA la Dk. Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kuhusishwa na uuzaji ‘kiholela’ wa viwanja 200 mali ya jumuiya hiyo, limechukua sura mpya, anaandika Charles William.
Agosti 16, mwaka huu, James Rock Mwakibinga, kada maarufu wa UVCCM, alijitokeza na kukitaka chama chake kiwachukulie hatua kali baadhi ya viongozi wa kitaifa ndani ya umoja huo ambao wameshiriki vitendo vya ufisadi wa mali za chama, akiwemo Dk. Nchimbi.
“Kuna maeneo mengi ambayo Baraza Kuu halikuyagusa katika kikao hicho, mfano; hawakugusia vile viwanja 200 vya Temeke ambavyo vimeuzwa kinyemela na Dk. Nchimbi na kwa sasa vimebakia vinne tu,” alisema.
Mwakibinga alikuwa akizungumzia kutokuridhishwa kwake na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na Baraza Kuu la UVCCM kwa watuhumiwa wa ubadhirifu wa mali za jumuiya hiyo, ambapo alidai kuwa, baadhi ya vigogo akiwemo Nchimbi wameachwa.
Ikiwa ni zaidi ya wiki moja sasa tangu Nchimbi kutuhumiwa, hatimaye amejitokeza na kueleza kusudio lake la kumfikisha Mwakibinga mahakamani kwa madai ya kumchafua kupitia tuhuma alizotoa.
Barua iliyoandikwa kupitia kampuni ya uwakili inayojulikana kama FK imesema, “sisi ni mawakili tunaoandika barua hii chini ya maelekezo ya Dk. Emmanuel Nchimbi (mteja wetu).
“Katika kikao chako na waandishi wa habari (16 Agosti mwaka huu), ulitoa tuhuma nyingi na nzito dhidi ya mteja wetu na uongozi mzima wa UVCCM ambapo ulitamka pamoja na mambo mengine tuhuma za kubuni ambazo haukuwa na uhakika nazo wala uthibitisho wake.”
Barua hiyo inanukuu baadhi ya maneno yaliyosemwa na Mwakibinga dhidi ya Dk. Nchimbi, yakiwemo haya; “kuna mtandao wa wezi na wabadhirifu wa mali za UVCCM unaofanywa na vijana pamoja baadhi ya watendaji, na ujangili huu unaaanzia katika Baraza la Wadhamini.”
Huku ikieleza kuwa, maneno yaliyosema na Mwakibinga yalilenga kuonyesha Dk.Nchimbi ni mwizi, jangili, hatari, asiyefaa kuwa kiongozi na asie na maadili na inahitimisha kwa kusema;
“Kutokana na sababu tulizotaja, tumeelezwa na mteja wetu kwamba, uchukue kila hatua itakayosafisha jina lake hasa kwa kuitisha mkutano mwingine na wanahabari mara moja na ukanushe tuhuma ulizotoa na kuomba radhi.
Pia ufute na kuondoa taarifa iliyomkashifu katika vyombo vyote vya habari pamoja na mitandao ya kijamii na umlipe haraka iwezekanavyo mteja wetu fidia ya shilingi 2.5 bilioni.
Wakati Dk. Nchimbi akikusudia kumshitaki Mwakibinga, itakumbukwa kuwa, kijana huyo alipoitisha mkutano na wanahabari alidai kuwa anao ushahidi wote dhidi ya tuhuma alizozitoa na aliahidi kuweka wazi ushahidi huo iwapo watuhumiwa wangekanusha.
Dk. Nchimbi amewahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya nne, akihudumu katika wizara mbili tofauti katika kipindi cha zaidi ya miaka nane, lakini pia amekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Ruvuma kwa kipindi cha miaka 10.
Post a Comment