SAA tatu baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kusitisha maandamano na mikutano yake chini ya operesheni yaUmoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta), Jeshi la Polisi limewataka viongozi wa chama hicho waliokamatwa juzi kutokwenda kuripoti polisi, anaandika Faki Sosi.
Taarifa ya kutotakiwa kuripoti kesho kama iliyotakiwa awali, zimethibitishwa na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho Taifa na Mbunge wa Jimbo la Hai, Kilimanjaro.
Waliotakiwa kufika Makao Makuu ya Polisi kesho ni pamoja na Mbowe; Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa; Katibu Mkuu, Vicenti Mashinji na Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika.
Juzi jeshi hilo liliwakamata viongozi hao wandamizi wa chama hicho wakati wakiendelea na kikao chao cha Kamati Kuu (CC) kwenye Hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilieleza kwamba, katika kamatakamata hiyo, mtafaruku mkubwa ulizuka baada ya viongozi wa jeshi hilo kutaka Chadema, kusitisha kikao chake cha CC, kilichokuwa kikiendelea hoteli hapo.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema zilieleza, baada ya mabishano makali, Jeshi la Polisi liliamuru baadhi ya viongozi wa chama hicho, kufika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano na baada ya hapo, walitakiwa kuripoti kesho Septemba Mosi.
Hata hivyo, baada ya Chadema kuahirisha Ukuta leo,Simon Sirro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ametoa kauli ya kupongeza uamuzi huo.
“Nawashukuru sana viongozi hawa kwa uzalendo waliouonesha kwa kusimamisha mikutano na maandamano yao..,” amesema Siro.
Post a Comment