Na sasa, matokeo ya kimbunga cha uhakiki huo yameibua pigo la aina yake lililoanza kuwakumba watumishi hao, wakiwamo vigogo wanaoshikilia nafasi mbalimbali za juu katika taasisi na idara mbalimbali za Serikali.
Taarifa ambazo Nipashe ilizipata wiki hii kupitia vyanzo vyake na kisha kuthibitishwa jana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, ni kwamba tayari kuna orodha ya watumishi waliobainika kupata ajira wakitumia vyeti bandia na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea, huku hatua za kisheria na kinidhamu ziko mbioni kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa wote wa udanganyifu huo.
Katika uchunguzi wake, Nipashe ilibaini kuwa baadhi ya watumishi hao wakiwamo vigogo wanaojijua kuwa vyeti vyao vya kielimu vina utata, tayari wameanza kujiondoa wenyewe kinyemela kwa kuacha kazi ghafla wakihofia hatua za kisheria dhidi yao.
Operesheni kabambe ya kuhakiki uhalisia wa vyeti vya watumishi wote wa umma wakiwamo vigogo katika taasisimbalimbali ilishika kasi tangua kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli, lengo mojawapo likiwa ni kuongeza ufanisi katika kazi ya kuwatumikia Watanzania na pia kutoa fursa za ajira kwa wataalamu wa fani husika katika kila nafasi na siyo “wataalamu bandia”.
“Huu uhakiki umeleta balaa… kuna watumishi hawana amani wakihofia hatima yao kwa sababu wamekuwa wakitumia vyeti bandia kwa miaka mingi na badhi wanashikilia nafasi za juu zenye mishahara na marupurupu makubwa,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe na kuongeza:
“Hata hivyo, baadhi wamejua kuwa wako hatarini kuumbuka na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kutokana na kosa la kufoji (kughushi), na hivyo wameacha kazi wenyewe na wengine wengi wa aina hiyo wanaachia ngazi kimyakimya.”
PANGA KUTEMBEA NCHI NZIMA
Baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa vigogo na watumishi wengine kibao walioanza kupatwa na kimbunga cha matokeo ya uhakiki wa vyeti, ndipo Nipashe ilipohitaji ufafanuzi kutoka kwa Dk. Ndumbaro, ambaye alikiri kuwapo kwa watumishi wengi waliobainika kuwa na vyeti bandia na kwamba baadhi yao wameanza kujiondoa wenyewe.
Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, uchunguzi zaidi kuhusiana na watumishi na maafisa wa juu wa serikali walioingia kwenye mfumo wa ajira bado unaendelea nchini kote na kwamba, hakuna atakayesalimika ikiwa atakutwa na hatia hiyo.
Katibu Mkuu huyo alisema tayari wizara yake ina taarifa za kuacha kazi kwa baadhi ya watumishi wakihofia kuchukuliwa hatua kwa kujijua kuwa wana vyeti bandia, lakini hadi sasa wapo wengine wengi wanaoendelea na kazi huku wakisubiria kujua hatima yao kwa kuwa uchunguzi kuhusiana na jambo hilo bado unaendelea.
“Zipo taarifa za watu kuacha kazi na wengine bado wanasubiria kujua hatima yao kwa sababu uchunguzi unaendelea… kwa sasa ni vigumu kujua ni wangapi walioacha kazi kwa kuwa tunaendelea na uhakiki wetu,” alisema.
Aidha, akizungumza na Nipashe jana, afisa mmoja msaidizi wa Dk. Ndumbaro aliiambia Nipasahe kuwa idadi halisi ya watumishi walioacha kazi katika kipindi hiki cha uchunguzi wa vyeti itakuwa tayari wiki inayoanzia kesho. Dk. Ndumbaro ndiye aliyemtambulisha afisa huyo kwa Nipashe.
ILIVYOKUWA
Serikali ilianza kuweka wazi mikakati yake ya kuwabaini watumishi wenye vyeti bandia hivi karibuni, ikitangaza pia kuanza rasmi kwa kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote walioajiriwa kwa vyeti visivyo na sifa.
Iliwataka watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kazini kabla ya kubainika kwani watafukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kugushi.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma wakati wa majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako alisema serikali imedhamiria kuboresha kiwango cha elimu nchini na kwamba, hatua mojawapo inayochukuliwa ni kukagua uhalali wa vyeti vyote vya elimu kwa watumishi wa umma katika sekta ya elimu na sekta nyinginezo.
Tamko la Waziri Ndalichako lilizua hofu, hasa kwa watumishi walioingia kwenye mfumo wa ajira za serikali kupitia ‘vimemo’ kutoka kwa wakubwa huku wakiwa hawana sifa stahiki za kufanya kazi walizopewa.
Baada ya kutangazwa kwa oparesheni hiyo, matangazo ya kupotea kwa vyeti vya elimu katika vyombo mbalimbali vya habari yaliongezeka maradufu huku.
OPERESHENI YAGUSA KILA KONA
Hadi sasa, idara na taasisi mbalimbali za umma nchini kote zimeshafanya uhakiki kabambe wa vyeti vya kielimu na kitaaluma kwa watumishi wao, baadhi zikiwa ni halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Kwa mfano, katika waraka mmojawapo wa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kahyarara kwenda kwa wakurugenzi wengine, mameneja wa mikoa wa mfuko huo, maafisa wa wilaya na wafanyakazi wote, na ambao ulisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ukionyesha kuwa na kumbukumbu namba NSSF/HQ/C/03/7Vol.II/120, ilikumbushwa kwamba kwa kuzingatia maelekezo ya awali kupitia waraka wa Juni 13, kila mmoja wao alitakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vyake halisi vya elimu na fani walizosomea kufikia Juni 24, 2016. Na kwamba, yeyote asiyefanya hivyo asingelipwa tena mshahara kuanzia wa mwezi Juni mwaka huu hadi hapo atakapotimiza sharti hilo la kuwasilisha vyeti.
Waraka mwingine mmojawapo kati ya nyingi zilizosambaa kutoka kwa wakuu wa taasisi mbalimbali za umma kwenda kwa maafisa na wafanyakazi wengine wote ni ule uliotolewa Julai 25, 2016 na Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata.
Kupitia waraka huo, wafanyakazi wote wa TRA wametakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vyao halisi kwa wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu katika maeneo yao kufikia Agosti 15, 2016.
“Yeyote atakayeshindwa kutii agizo hili atawajibika mwenyewe,” inaeleza sehemu ya waraka huo wa Kamishna wa TRA kwenda kwa wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo. Panga dhidi ya watumishi waliogushi pia linatarajkiuwa kuwakumba watu walioomba kazi kupitia vyeti vya watu wengine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, aliwahi kuiagiza Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu (Utumishi) kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kutumia vyeti visivyo vyao ili kupata ajira serikalini.
Wakati msako wa watumishi wenye vyeti bandia ukiendelea, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), nalo lilitoa tamko zito lililowataka watu wote wanaojijua wazi kuwa wanamiliki vyeti bandia kujisalimisha wenyewe. Tamko hilo lilitolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
“Necta ndiyo yenye dhamana ya kutoa vyeti vyote vya watahiniwa wanaomaliza mitihani ya Taifa nchini, kulikuwa na changamoto ya vyeti feki (bandia) kwa kipindi kirefu sasa wanaojijua wajisalimishe maana watakamatwa tu,” alisema Dk. Msonde, akigusia tatizo la kushamiri kwa vyeti bandia.
Post a Comment