Wakati CCM ikitangaza makatibu wapya wa mikoa na wilaya, chama hicho kimesema kitahakikisha kinajenga urafiki usio na shaka kwa kuchunguza uadilifu wa wahisani watakaotaka kukichangia chama hicho, kabla ya kupokea michango yao.
Uamuzi huu umefikiwa na CCM kutokana na kile kinachoonekana chama kutaka kisitekwe na wafadhili kutokana na nguvu yao ya fedha. Hii ni pamoja na kuondoa uwezo wa wafadhili kuamua nani agombee nafasi ipi.
Kukiweka mkononi chama kutokana na michango inayotolewa na marafiki hao ambao huwa na uwezo wa kushawishi nani agombee nafasi ipi.
CCM pia imeamua kuendesha shughuli zake muhimu, kama uchaguzi mkuu kwa kutumia fedha zinazotokana na vyanzo vyake vya ndani.
“Chama kitaendelea kupokea michango kutoka kwa matajiri wanaotaka kukiunga mkono kwenye miradi na shughuli mbalimbali,” alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mahojiano maalumu na waandishi wa Gazeti la Mwananchi.
“Marafiki wa CCM bado wapo na wataendelea kukisaidia chama, ila sasa ni lazima tujiridhishe kwamba si wakwepa kodi, hawauzi unga na wanafanya biashara halali.
Polepole pia alisema CCM itataka kujihakikishia kuwa misaada ya wafadhili hao haikigawi chama.
CCM imekuwa ikisemekana kutegemea kwa kiasi kikubwa michango ya wafadhili kujiendesha, hasa inapotaka kuitisha vikao vyake vya juu kama Mkutano Mkuu na Halmashauri Kuu.
Pia chama hicho kinategemea misaada ya marafiki zake katika shughuli za uchaguzi, ikiwa ni pamoja na uchapishaji vifaa vya kampeni kama fulana, vipeperushi na khanga.
“Yote yaliyoafikiwa hayakufanywa kwa kumtazama mtu,” alisema Polepole.
“Tumeweka mfumo mzuri utakaodhibiti rushwa kwa kuwa awali wapo waliothubutu hata kuchapisha kadi za uanachama na kuunda makundi yao ndani ya chama.”
Wakati ikitegemea wafadhili kuendesha shughuli zake, CCM inamiliki mali nyingi kubwa kama majengo ya kukodisha, viwanja vya michezo na kumbi za mikutano
“CCM ina mali zake yenyewe wala haijapewa na Serikali kama wengi wanavyodhani. Tumefanya mabadiliko ya katiba ambayo yanalenga kuongeza usimamizi wake,” alisema Polepole.
Ili kufikia uwezo huo, Polepole alisema utaratibu wa kuhakiki mali zote za chama umewekwa na utahusisha mapato na matumizi kwa namna ambayo ziada itapelekwa makao makuu kwa mipango ya kitaifa.
Polepole alisema hadi mwaka 2011, CCM ilikuwa inamiliki viwanja 32 vya michezo na kati ya hivyo, 22 vinatumika kwa mechi za soka za ligi kuu pamoja na ligi daraja la kwanza.
Kutoka kwenye vitega uchumi vyote walivyonavyo, alisema kutakuwa na mapato ambayo yanapelekwa makao makuu huku wanaovisimamia wakitoa kiasi kinachotosha kukidhi gharama za uendeshaji.
Polepole alisema mkakati mwingine wa chama hicho ni kuongeza thamani ya mali ilizonazo ili zitumike au kukodishwa kulingana na hali ya soko la sasa pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Alisema vikao vya juu vya chama hicho vimekuwa vikighartimu fedha nyingi.
Alisema kikao cha Halmashauri Kuu, ambacho kabla ya mabadiliko ya katiba ya CCM kilikuwa na wajumbe takriban 400, kilikuwa kikitumia Sh600 milioni lakini baada ya kuwapunguza mpaka 163, sasa kitatumia Sh100 milioni tu.
“Halmashauri inakutana mara tatu kwa mwaka. Unaweza kuona ni kiasi gani kitaokolewa kwa mabadiliko haya ambayo hayajaathiri uwakilishi wa wajumbe,” alisema Polepole.
Kwa hatua hizo, alisema katika mkakati wa chama kuhakikisha kinaongeza uwajibikaji na kuziba mianya yote ya rushwa, ipo mikakati thabiti.
Licha ya hatua hizo, Polepole alisema kingine kilichofanywa na chama hicho tawala ni kuwaondoa makamanda na makatibu wasaidizi wilaya na mkoa ambao walikuwa wanalipwa mishahara kwamba ni moja ya dhamira za kupunguza matumizi.
Sambamba na marekebisho hayo alisema ajira za watumishi wa jumuiya zake; Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Wanawake (UWT) litafanywa chini ya sekretarieti moja tofauti na ilivyokuwa awali.
Licha ya watumishi hao wa chama, alisema hata gharama za mikutano zimepunguzwa baada ya kushusha idadi ya wajumbe watakaokuwa wanahudhuria.
Download Video ya Gwajima
" imageanchor="1" style="margin-left: 1em; margin-right: 1em;">
Mabadiliko
Katika mabadiliko hayo yaliyopitishwa na Mkutano Mkuu, CCM imeondoa kofia mbili za uongozi kwa wale wanaoshika nafasi za utendaji.
Lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano ataendelea pia kuwa mwenyekiti wa chama.
“Mwenyekiti ndiyo kichwa, ndiye kiongozi kwenye chama chetu. Tumekubaliana tunampa dhamana ya kuwa mgombea wa chama chetu ili atupe uongozi mmoja wa chama na atumie nafasi hiyo kuongoza Serikali,” alisema Polepole.
Alisema nchini China mwenyekiti wa chama ni rais wa nchi hiyo, lakini chini ya cheo hicho watendaji wengine wote hawaruhusiwi kulimbikiza mamlaka.
“Bado tunahitaji mtu mmoja atubebee dhamana ya nchi na huu ni msimamo tuliokubaliana. Rais wetu, ndiye tunampa uenyekiti wa chama. Ni ku- maintain na kuhuisha ukubwa wa nchi na chama,” alisisitiza Polepole.
“Diwani ambaye amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa halmashauri ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya kwa nafasi hiyo na anaweza akagombea nafasi kwenye kamati ya siasa ya mkoa pia,” alisema.
Akiwa na nafasi hizo zote na akakosea, alisema hakuna kamati inayoweza kumuwajibisha kwa sababu kote ni mjumbe.
Urais
Akizungumzia madai ya kuwapo kwa mpango wa kuweka pingamizi la kugombea bila kupingwa katika kipindi cha pili kwa Rais aliyepo madarakani, Polepole alisema hayana ukweli wowote.
“Hili jambo la kupinga ni uongo. Hakuna kikao chochote tulichojadili suala la kugombea kwa maana ya kuomba nafasi ya kupeperusha bendera mwaka 2020,” alisema.
Alisema suala hilo lipo kwenye utamaduni wa CCM wa siku nyingi kwamba Rais aliyepo anapitishwa kwa muhula unaofuata ingawa hakuna anayezuiwa kuchukua fomu ya kumpinga.
“Kila baada ya miaka mitano watu wanaruhusiwa kuchukua fomu. Hata mwaka 2010 walifanya hivyo. Lakini kwa aliyefanya kazi nzuri tutampa tena nafasi. Hatujaondoa haki hiyo ya kidemokrasia ndani ya chama,” alisema.
CCM yapanga upya makatibu wa mikoa, wilaya
Wakati huo huo CCM jana kilitangaza safu yake mpya ya watendaji katika ngazi ya mkoa na wilaya, baada ya kukamilisha uteuzi wa makatibu wake katika ngazi hizo mbili kwa upande wa Bara, huku Zanzibar ikiwekwa kiporo.
Uteuzi wa makatibu hao ulitangazwa jana na Polepole, alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Katika uteuzi huo wapo watendaji waliopandishwa kutoka ngazi ya wilaya kwenda mikoa, huku wengine wakihamishwa katika vituo vyao vya kazi.
Ingawa uteuzi wa makatibu wa mikoa yote 31 tayari umeshakamilika, lakini Polepole alitaja makatibu wa mikoa 25 tu huku wa mikoa mitano ya Zanzibar akisema yatatangazwa baadaye sambamba na makatibu wa wilaya zote za Zanzibar, ambao bado hawajateuliwa.
Polepole alisema kwamba watendaji hao kwa upande wa Zanzibar watatangazwa baada ya kumalizika kwa tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, na hali ya kisiasa ya Zanzibar.
“Uteuzi huu umezingatia maadili, weledi, jinsia na mpango wa kuachiana vijiti kwa kuzingatia rika.”, alisema Polepole.
Polepole alifafanua kuwa makatibu wa mikoa 11 na makatibu wa wilaya 75 ni wapya.
Wateule hao wapya hawajawahi kushika nafasi hizo bali wamekuwa wakitumika ndani ya chama katika nafasi mbalimbali na kwamba zaidi ya asilimia 30 ni wanawake.
“Makatibu wengi tuliowateua ni wapya, hatuwezi kufanya mageuzi ya kuwa na CCM mpya na upya huo usionekane. Mageuzi ni fikra” alisema.
Alifafanua kuwa lengo la kuteua watendaji hao wapya ni kuendana na dhana ya CCM mpya kutokana na mpango wa mageuzi yanayofanywa ndani ya chama hicho, ili kuingiza mawazo mapya yatakayoshirikiana na yale ya wazoefu.
Alisema kuwa jukumu la kwanza la watendaji hao ni kusimamia uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya chama hicho, unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Awali, Polepole alisema kufuatia mageuzi yanayaoendelea ndani ya chama hicho nafasi za utendaji zitakuwa zinatangazwa ndani ya chama kwa kuwapa fursa wenye sifa za kitaaluma, waadilifu, weledi na uzoefu.
Alisisitiza kuwa wanataka mtawanyiko wa jinsia na viongozi wanaokidhi misingi ya kuendana na utamaduni wa kupokezana vijiti kwa marika ili vijana waweze kujifunza na kupata uzoefu wa uongozi kutoka kwa viongozi watu wazima waliopo.
Post a Comment