
Sambamba na viongozi wa WETCU kutimuliwa ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha, serikali pia imeliagiza
Jeshi la Polisi mkoani Tabora kuwakamatwa viongozi hao.
Mbali na viongozi kusimamishwa, Majaliwa alitangaza juzi katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Isike Mwakiyungi mkoani
Tabora kuwa Rais ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku, Vita kawawa na Mtendaji Mkuu wa bodi, Wilfred Mushi.
Viongozi wa WETCU ambao Waziri Mkuu aliagiza wakamatwe ni Mwenyekiti,. Mkandara Mkandara, Makamu Mwenyekiti,.
Msafiri Kassim, Mkaguzi wa Ndani na Mhasibu Mkuu huku watumishi wa idara ya uhasibu wakisimamishwa hadi uchunguzi utakapokamilika.
Waziri Mkuu alisema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na TTB, jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.
“Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea Sh. bilioni 15 ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni Sh. bilioni 10 ambazo hawajazikatia risiti.
“Wakati wanachama ambao ni wakulima wakiendelea kutesema, WETCU walinunua gari la Sh. milioni 269 kinyume cha maelekezo ya Mkutano Mkuu wa wadau ambao ulipitisha zitumike Sh. milioni 40 tu,” alisema.
Pia alisema chama hicho kimesababisha kupungua kwa uzalishaji kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na menejimemti mbovu jambo ambalo limechangia wakulima wa tumbaku kukosa tija.
Aidha, alisema WETCU imekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha ambapo alitolea mfano suala la ukarabati wa ofisi tatu ikiwemo ya makao makuu ambayo ilipangwa ikarabatiwe kwa Sh. milioni 33 wakatumia Sh. milioni 170 na ofisi za Tabora na Urambo zilipangiwa Sh. milioni tano kila moja na hazikukarabatiwa.
Wakati hayo yakifanyika, wakulima wa tumbaku kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Tabora, wameelezea kufurahishwa na uamuzi wa kutimuliwa viongozi wote wa (WETCU) uliofanywa na serikali.
Wakulima hao walisema umaskini walio nao umechangiwa na viongozi wa Bodi hiyo kwani walishindwa kabisa kusimamia maslahi yao huku wakilipana posho nene za jasho la wakulima.
Walisema mpaka sasa wanaidai bodi hiyo mabilioni ya fedha ambazo ni sehemu ya malipo yatokanayo na mauzo ya tumbaku yao na hapakuwa na mkakati wowote wa kulipa fedha hizo kwa wakati huku wakulima wakiendelea kukatwa madeni ya pembejeo.
Mkulima wa kijiji cha Mole wilayani Sikonge, ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, alipongeza uamuzi huo kwa kuwa viongozi hao walikuwa wabinafsi na kujifanya miungu watu hali iliyopelekea kulundikana kwa madeni yao.
Mkulima mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jilala kutoka wilayani Kaliua alisema WETCU walikuwa wajanjawajanja ndio maana hata vikao vya mkutano mkuu wa wakulima wa zao hilo vilikuwa vikikaliwa na Mwenyekiti pekee na hawakuwa tayari kukoselewa.
Mwenyekiti wa Wakulima binafsi wilayani Kaliua, Moris Rubundi, mkazi wa Usinge, alipongeza hatua iliyochukuliwa na serikali kwa kuwa WETCU iliwaonea sana na ilikuwa haiwatendei haki.
Alisema kitendo cha baadhi ya wakulima kuamua kujitenga na ushirika huo kilisababishwa na viongozi hao kutumia fedha zao vibaya na kushindwa kusimamia ipasavyo maslahi ya wakulima wote huku wakinemeeka kwa jasho la wakulima.
Post a Comment