KATIBU Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda amesema afya ya Mwenyekiti wa Chama hicho, James Mbatia inaendelea vizuri na matarajio yao ni kumwona akishiriki Bunge la Bajeti linaloanza leo, Dodoma.
Aidha, Danda amesema chama hicho hakirudi nyuma kujijenga na kuwa watu wanaofikiria kuwa kitaharibu malengo yake hawatafanikiwa.
Katibu huyo alisema hayo jana alipozungumza na kubainisha kuwa kwa matibabu anayopata Mwenyekiti wao yanamfanya aendelee vizuri na afya yake inazidi kuimarika.
“Tangu atoke kwenye matibabu amekuwa akiimarika na kwa sasa hata magongo hatumii kutembea na naamini atashiriki vikao vya Bunge,” alisema.
Alisema wamejiwekea mikakati ya kurejesha heshima ya chama, hivyo watu wanaotumika kuharibu mwelekeo wa chama hawatakubalika.
Katibu Mkuu alisema katika kuonesha dhamira ya kujenga chama wamemfukuza aliyekuwa mwanachama wao, Faustine Sungura baada ya kubaini kuwa hana nia njema na chama hicho.
Alisema Sungura amekuwa akishirikiana na watu kujaribu kuhuju chama, hivyo wasingeweza kumvumilia.
“Sungura amekuwa akitumika na bahati nzuri hakuwa na cheo hivyo hana madhara lakini katika kurejesha heshima ya chama Kamati Kuu ilivyokutana hivi karibuni iliamua kumfukuza NCCR-Mageuzi,” alisema.
Kwa upande mwingine alisema chama hicho hakina mpango wa kufungua kesi ya kupinga mchakato wa uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kwa kuwa wagombea wa vyama vya CUF na Chadema ni wana Ukawa wenzao.
Post a Comment