Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

HIVI NDIVYO SAMAKI WA MAGUFULI WALIVYOZUA KIZAAZAA KIZITO LEO BUNGENI.

MBUNGE wa Nungwi (CUF), Yussuf Haji Khamis, ameibua Bungeni samaki waliokamatwa mwaka 2009 katika Bahari ya Hindi, maarufu kama ‘Samaki wa Magufuli’.

Katika kuibua suala hilo, mbunge huyo alihoji jana ni lini serikali itarudisha zaidi ya Sh. bilioni mbili ambazo ni thamani ya samaki tani 296.3 waliokamatwa wakati huo.

Akiuliza swali jana bungeni, mbunge huyo alisema mwaka 2009 serikali ilikamata meli ya uvuvi MFV Tawariq, Nahodha wake Tsu Chin Tai na watu wengine 36 na hatimaye kushtakiwa mahakamani.

“Kwa amri ya mahakama, samaki tani 296.3 wenye thamani ya Sh. 2,074,000,000 waligawiwa bure na meli hiyo ilizama ikiwa inashikiliwa. Watuhumiwa wawili walihukumiwa kifungo, walikata rufani Mahakama ya Rufani na mwaka 2014 waliachiwa huru,” alisema.

Akijibu swali hilo, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Angella Kairuki, alisema Machi, 2009 kikosi kazi kilichokuwa kikifanya doria katika ukanda wa kiuchumi wa bahari hiyo kilikamata meli hiyo.

Alisema meli hiyo yenye namba za usajili 68 BU YOUNG ilikamatwa ikivua katika bahari hiyo bila kibali na ilikuwa ikitumia jina la Tawariq 1 na Tawariq 2 ili kuficha jina halisi na kuendelea kufanya uvuvi haramu.

“Nahodha wa meli hiyo na wenzake walishtakiwa Mahakama Kuu, kesi ya jinai ambayo nahodha na Zhao Hanquing aliyekuwa wakala wa meli hiyo walitiwa hatiani, walikata rufani na mahakama ilibatilisha na kufuta mwenendo mzima wa kesi,” alisema Kairuki.

Alibainisha kuwa mwenendo mzima wa kesi ulifutwa kutokana na kasoro katika taratibu za kuwafungulia mashtaka, hivyo hawakuwahi kushinda kesi na Mahakama ya Rufani haikuwahi kuwaambia wako huru kwa sababu hawana hatia.

Kairuki alisema baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi wa Mashtaka alifungua mashtaka upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baadaye kuondoa mashtaka dhidi yao mwaka 2014.

Hata hivyo, alisema baada ya mwama jana Wakili Ibrahim Bendera alifungua maombi katika Mahakama Kuu akimwakilisha Said Ali Mohamed ambaye hakuwa mmoja wa washitakiwa katika kesi ya msingi, akiomba apewe meli au Dola za Marekani milioni 2.3 (zaidi ya Sh. bilioni 4.6) kama thamani ya meli na Sh. bilioni 2.074 kama thamani ya samaki.

Kadhalika, alisema Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, ilikubali hoja ya Jamhuri na kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa hayakustahili. “Kutokana na mwenendo wa kesi hii, hili ni suala la kisheria na wahusika wanaweza kuendelea kulishughulikia kupitia mahakamani,” alisema Kairuki

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top