LICHA ya viongozi wa dini kuepusha maafa kwa kushauri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kusitisha maandamano na mikutano yake, wameonekana wapuuzi, anaandika Dany Tibason.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umeeleza kuwa, usuluhishi wa kisiasa kati ya Chadema na chama tawala (CCM) si kazi ya viongozi wa dini na taasisi nyingine nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Shaka Hamdu Shaka, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma.
Shaka wamewataka viongozi hao kuacha kabisa kumsumbua Rais John Magufuli ama kumpotezea muda kwa kutaka kujadili usuluhishi wa kisiasa kwa kuwa, wao si wanasiasa.
Mbele ya waandishi wa habari jana, Mbowe alisema maandamano na mikutano inayotaribiwa na chama chake chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukawa), yape pale pale na kwamba yamesogezwa mbele mpaka Oktoba Mosi mwaka huu.
Alisema, uamuzi wa chama hicho ni kusogeza mbele maandamano hayo ni kupisha mazungumzo baina ya Rais Magufuli na taasisi mbalimbali nchini zilizoomba maandamano na mikutano hiyo kusogezwa mbele.
Alisema, Chadema kimeridhia maombi ya kusitisha maandamano na mikutano hiyo nchi nzima yaliyotolewa na viongozi wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wa taasisi za kirai.
Tarehe 27 Julai, mwaka huu Chadema kupitia Mbowe kilitangaza kuwa, Septemba 1 mwaka huu, kitazindua operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ikiwa ni maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichoketi wa siku mbili.
Akizungumza na wanadishi wa habari Dodoma mbali na kushambulia viongozi wa dini pia wamezitaka asasi mbalimbali na mashirika ya hiyari kuachana na mawazo ya kumtafuta rais kwa lengo la kufanya mazungumzo ya kisiasa.
Wameshauri taasisi hizo kutumia muda huo kwa ajili ya ya kuzungumzia masuala ya maendeleo tofauti na masuala ya kisiasa.
Pia UVCCM wamesema, serikali haitakuwa na mazungumzo, majadiliano kati ya Serikali ya CCM na Chadema.
“UVCCM tunatamka bayana kuwa, hakuna mazungumzo, mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM na Chadema.
“Tunaomba Serikali ya Rais John Magufuli iendelee na mikakati yake ya kisera ili kushamirisha maendeleo ya kiuchumi na juhudi za utekelezaji wa kuiletea mabadiliko nchi yetu ili kuwa ya viwanda sanjari na kupambana na maadui umasikini, ujinga na maradhi,” amesema.
Kwa mujibu wa Shaka, Tanzania ni nchi ya amani ambayo haihitaji kuwepo kwa mazungumzo yoyote ambayo yanalenga kuleta amani.
Shaka mbele ya waandishi wa habari amesema, hoja zilizotolewa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa ChademaTaifa wakati akisitisha Ukuta hazima mashiko.
“Hoja za Mbowe ni utapeli wa kisiasa, usanii na mwendelezo wa tamthilia ya kisiasa inayoendelea kufanywa na viongozi wa chama hicho kwa dhumuni la kujitafutia umaarufu wa kisiasa,” amesema.
Kiongozi huyo amesema, kauli iliyotolewa na Mbowe kuwa wamesitisha maandamano kwa ajili ya kusikiliza ushauri wa viongozi wa dini na asasi mbalimbali si ya kweli.
“Sisi UVCCM tunajiuliza ni lini Chadema wamekaa na viongozi wa dini wakati viongozi hao wa Chadema walikuwa wakimbeza Rais Magufuli kuwa ni dikiteta? walishariana na viongozi wa dini?
“Kwetu UVCCM wakiwemo wananchi wema wapenda amani na utulivu, viongozi wa mashirika ya hiari na kiraia na kijamii na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini, hatuwezi kusimama hadharani na kuithibitishia dunia kwamba, Tanzania kuna jambo ambalo linaitwa mgogoro wa kisiasa ambao unahitaji yafanyike mazungumzo, majadiliano hadi kufikia mapatano” amesema Shaka.
Post a Comment