Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

Tanzania kinara Afrika huduma za kifedha kwa njia ya simu


Dar es Salaam.Utafiti mpya umeonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kwa kuwa na mazingira bora ya huduma za kifedha kwa njia ya simu.
Ripoti ya utafiti huo iliyotolewa na Taasisi ya Uchumi (EIU) ilibaini kuwa Tanzania ni nchi ya sita duniani katika matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya teknolojia ya simu.
Akizungumza katika warsha ya kujadili uchumi shirikishi jana, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu alisema Tanzania imeshika nafasi hiyo kwa sababu imeboresha mazingira ya huduma za kifedha kwa njia ya simu.
“Tumechukua msimamo wa kuruhusu teknolojia iongoze. Kwa kutumia simu ya mkononi tumeweza kumfikia mtu yeyote bila kujenga matawi ya benki,” alisema.
Gavana Ndulu alisema simu za mkononi zimekuwa njia rahisi ya kuwafikia Watanzania wote na kwa gharama nafuu.
Kwa sasa Tanzania ina mawakala wa mitandao ya simu zaidi ya 270,000 ambao wamesambaa nchi nzima lakini kuna matawi ya benki chini ya 6,000.
“Ukiangalia wepesi wa matumizi ya simu unaona jinsi ambavyo ni rahisi kuwafikia Watanzania na kuwapa huduma za kifedha,” alisema.
Kuhusu madhara ya teknolojia ya simu za mkononi, Profesa Ndulu alisema Serikali ilijadili na kuona ni vyema kuendelea kwanza na matumizi hayo wakati usalama na uhakika wa huduma hizo ukitafutwa.
Katika warsha hiyo, ripoti ya uchumi jumuishi kwa mwaka 2014 ilisomwa na kubaini kuwa asilimia 40 ya Watanzania kwa sasa wanatumia huduma za kifedha kwa njia ya simu.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya simu yameongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2011 hadi 40 mwaka 2014.
Hata hivyo, Profesa Ndulu alikanusha uwezekano wa benki kufa kutokana na matumizi ya simu za mkononi: “... Kwa kila shilingi iliyopo kwenye simu ipo pia kwenye benki, kwa hiyo wajibu wa benki bado upo palepale.”
Meneja Uchumi na Kilimo wa Benki ya Dunia, Marvin Taylor alisema Tanzania imekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika kipindi kifupi.
Alisema katika tafiti alizofanya, amebaini kuwa familia ya kipato cha chini nchini, haina tofauti na familia ya kipato cha chini katika nchi nyingine zilizoendelea.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top