Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

HII NI NOUMA KAULI YA LEMA LEO YALITIKISA JIJI LA ARUSHA WANAE WAFANYA KUFURU NZITO JUKWAANI LEO HII.


MBUNGE wa Arusha Mjini Godbelss Lema, amechokoza mapya jijini Arusha, kwa kuwapandisha jukwaani wanaye wawili na kudai kama kushtakiwa kwa amri ya polisi iliyomtaka awe mzungumzaji pekee katika mkutano wa hadhara, basi waunganishwe wote na kushakiwa. Lema alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika shule ya Msingi Ngerenaro kwa ajili ya kusalimiana na wananchi pamoja na wapigakura wake, baada ya kuachiwa na mahakama kwa dhamana wiki iliyopita.
Katika barua ya polisi ya kumruhusu kufanya mkutano jana, walimtaka kuwa mzungumzaji pekee katika mkutano huo, lakini Lema akasema amewapandisha jukwaani watoto hao ili kama kumshtaki basi waunganishwe wote.
Baada ya kupandishwa jukwaani, Lema aliwaita watoto wake (Briliant na Terence) ambao waliwasalimia wananchi kwa nyakati tofauti kwa salamu za Chadema wakianza kwa kuzungusha ngumi na kutamka People’s.
Wakati wakisalimia wananchi, watoto hao kila mmoja kwa wakati wake waliimba wimbo wa ‘CCM kwisha, kwisha kabisa. Mbende mbende, nyang’a nyang’a…kifo cha mende, chalii; hakuna kulala mpaka kieleweke,’ na kuwafanya mamia ya watu waliokuja kusikiliza mkutano huo kuangua kicheko.
Akihutubia mkutano huo, Lema aliyekuwa mahabusu miezi minne kabla ya kuachiwa kwa dhamana na mahakama, alisema hajaingiwa baridi kufuatia kukaa kwake mahabusu.
Alimwomba Mungu kuwasamehe wote waliosuka mpango wa kumweka mahabusu na kuweka mapingamizi ya kesi yake ili aendelee kusota mahabusu, kwa kuwa wamemfanya kujua jinsi watu wanavyoteseka kwa kukosa haki.
Alimtaja Wakili msomi Median Mwale ambaye yupo mahabusu kwa miaka sita sasa kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha.
Alisema kukaa kwake mahabusu kutamfanya akienda bungeni kutoa mchango mkubwa kuhusu kurekebisha sheria wanazozitunga ili ziweze kutenda haki.
Alisema kwa mfano, akiwa mahabusu alishuhudia watoto wadogo wenye umri wa miaka 14 hadi 16 wakiwa wamefungwa mwaka mmoja hali ambayo alisema, watalawitiwa na kujifunza ukatili.
“Nikienda bungeni mchango wangu utakuwa wa magereza na watoto wadogo ili kulinda haki zao,” alisema.
Badala yake alisema yupo moto kupigania haki na demokrasia nchini.
“Sijaingiwa baridi, nimeingia moto…kama walifikiri kunitisha kiasi hicho nitaingia woga, wamempiga chura teke,” alisema na kuongeza: “Nimeapa na wala sitarudi nyuma.”
“Hata wabunge wote wakirudi nyuma, mimi nitaendelea kusonga mbele kupigania haki na demokraia ya nchi hii.
“Nyuma yangu mnataka nini, mimi nataka tuwe sambamba,” alisema Lema ambaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa kipindi cha pili kuanzia mwaka 2010.
Alisema hata Rais John Magufuli ametamka kwamba hajaribiwi, lakini wao hawatamjaribu isipokuwa watafanya kweli kutetea na kupigania haki za wananchi wa taifa hili.
Alisema hakuna dhambi kubwa kwa binadamu kama uoga na akataka wabunge na watu wengine wanaomweleza kuwa wapo nyuma yake, waache kusema hivyo, badala yake aliwataka wawe sambamba naye.
Huku akiwatetea polisi, ofisi ya mwendesha mashtaka, mahakama kuwa wanalazimika kupindisha haki kutokana na woga walionao kwa watawala, aliwalaumu akisema: “Hakuna dhambi itakayopandwa mmoja akavuna haki.”
“Hawa polisi wala msiwalaumu, RCO pia msimlaumu, maafisa wa mahakama wala msiwalaumu ni woga tu umewajaa,” alisema.
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kuwa fedha za bajeti ya mwaka 2016/17 utekelezaji wake haujafikia asilimia 40 huku fedha nyingi zikitumika nje ya bajeti, ikiwamo kuhamishwa kwa wizara kwenda Dodoma.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa bajeti ya mwaka huu inaelekea mwisho, lakini utekelezaji wake haijafikia asilimia 40.
Kwa mujibu wa Dk. Mashinji, asilimia 60 ya bajeti ya mwaka 2016/2017 haijatekelezwa na kwamba ni hatari kwa maendeleo ya taifa.
Alisema licha ya serikali kusema imekusanya mapato mengi, lakini bado kuna tatizo katika utekelezaji wa bajeti.
Alitolea mfano, uamuzi wa kuhamia Dodoma kuwa umeathiri kwa kiasi kikubwa bajeti ya nchi kwa sababu hazina haikupata muda wa kukaa na kupitia marejeo ya bajeti.
Aliongeza:” Huu ucheleweshaji wao una maana kwamba wanataka kubaki kwenye muda ule ule ambao wameupanga kuwa bajeti ya taifa lazima ianze Julai 1, lazima muda uwe umefupishwa na kama muda utafupishwa ina maana kuna baadhi ya vitu vitakuwa vinapitishwa bila wabunge wetu kupata fursa ya kuvijadili.”
Alisema: “Kama serikali inashindwa kuliwezesha bunge ina maana kuwa bunge litakuwa linakimbizana kufupisha mambo ili kuendana na muda na huu ni mwendelezo wa serikali kuhakikisha kuwa inalibana bunge ili wasiweze kuisimamia vizuri serikali.”
Alisema kitendo hicho kina athari japo kuna watu wanafurahia mpango wa kuhamia Dodoma ni jambo la muda mrefu tangu ilipotangazwa Dodoma kuwa mji mkuu na sheria ya kuifanya kuwa mji mkuu bado haijakamilika.
Alisema kulikuwa na fursa ya kufanya jambo hilo kwa hatua ili kukamilisha mchakato wa kuhamisha ofisi bila kuwapo na athari yoyote.
Dk. Mashinji alidai kumekuwa na mpango wa kutolewa fedha nje ya kasma za bajeti iliyopangwa na bunge.
“Lakini ukiangalia vitu vyote vinakwenda nje ya mpango fedha zilizokuwa kwenye mpango, siamini kama zimeshapelekwa tuulizane zile Sh. milioni 50 za kila kijiji kuna ambaye anajua ni kiasi gani kilichopelekwa. Sisi tumetuma watu wetu wamefuatilia hakuna fedha iliyopelekwa, lakini kuna fedha zinatolewa nje ya mpango,” alidai.
Alisema bajeti inayokwenda kila wizara ni majanga na kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupatiwa fedha ndogo ikilinganishwa na bajeti iliyopitishwa.
Dk. Mashinji alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wametengewa Sh. bilioni 11.18 kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC), jambo la kushangaza fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Sh. bilioni 1.5 ambazo zitanunua magari mawili ya zimamoto.
Aidha, alisema fedha za uendeshaji ni Sh. bilioni 3 zimetengwa endapo ikatokea majanga ya moto hakuna fedha za kununulia dawa za kuzimia moto.
Aliwataka wabunge kuweka itikadi zao pembeni kwa ajili ya kuisimamia na kuiwajibisha serikali kwa mujibu wa katiba katika utekelezaji wa bajeti pamoja na kuhakikisha maazimio yote ya bunge yanatimizwa.
Alisema bunge lisimame kama mhimili na kutekeleza majukumu yake, lisikubali kushushiwa hadhi kwa kuwa ni wawakilishi wa wananchi.
Imeandikwa na John Ngunge na Beatrice Shayo

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top