Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

Makada Hawa Wanane wa CCM Watiwa Mbaroni kwa Rushwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inawashikilia makada wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa tuhuma za kujihusisha na utoaji rushwa katika matukio tofauti ya mchakato wa kura za maoni za ubunge na udiwani, jijini Dar es Salaam na Lindi.

Kadhalika Takukuru inashikilia kiasi cha Sh. 1,677,000 kilichokutwa kwa makada hao kupitia mtego uliowekwa kwenye majimbo ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Makada hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) kata ya Goba, Pili Mustafa, aliyekamatwa  saa 3 usiku akiwa na Sh. 1,330,000, Rehema Luwanja, anayegombea udiwani kata ya Goba na Sh. 95,000, huku akiwa ameshagawa 110,000.

Wengine ni Katibu Itikadi wa CCM kata ya Kibamba, Babu Kimanyo, aliyekamatwa saa 4:30 usiku akiwa na  Sh. 252,000 na tayari alishagawa sh. 330,000, Katibu CCM kata ya Kibamba, Elias Nawera ambaye anagombea Ubunge Kawe, Siraju Mwasha anayegombea udiwani Msigani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Denis Manumbu, alisema kuwa mbali na watuhumiwa hao, wamepokea malalamiko 28 yanayohusu rushwa ambayo wanayafanyia uchunguzi ili hatua zichukuliwe.

Alisema katika kipindi hiki cha kura za maoni za kuwapata wagombea katika ngazi ya udiwani na ubunge katika vyama vya siasa majimbo manne ya Wilaya ya Kinondoni, ofisi yake imepokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi zinazohusu vitendo vya rushwa.

Manumbu alisema vitendo hivyo vinafanywa na watangaza nia na wapambe wao na baada ya kupitia taarifa hizo ofisi ilizifanyia kazi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao na kuwahoji.

Alisema ofisi yake ina mamlaka kisheria ya kumuita mtu yeyote kutoa maelezo ili kusaidia uchunguzi wa tuhuma husika na mamlaka hayo kwa mujibu wa kifungu cha 10(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, atakayekiuka wito huo atakuwa amekwenda kinyume cha sheria.

Hata hivyo, alisema Takukuru inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na hawatasita kumchukulia hatua mgombea wa chama chochote na upelelezi utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo vya dola.

 LINDI WATIA NIA UBUNGE CCM WANASWA
Huko Lindi, Takukuru, imewakamata na kuwahoji wagombea wawili wa nafasi ya ubunge kupitia CCM kwa madai ya kutaka kuwahonga wajumbe, wakati wa mchakato wa kura za maoni.

Kamanda wa Taasisi hiyo, mkoani hapa, Stephen Chami, amewaambia waandishi wa habari kuwa, wagombea hao wamekamatwa usiku katika majimbo ya Lindi Mjini na Mchinga kati ya saa 5 usiku na 10-11 alfajiri ya kuamkia jana.

Aliwataja wagombea na majimbo wanayogombea katika mabano kuwa Mwekahazina wa Chama cha Walimu Taifa (CWT), Mohamedi Utali (Lindi mjini) na mbunge viti maalumu aliyemaliza muda wake, Fatuma Mikidadi (Mchinga).

Alisema, Utali alikamatwa maeneo ya Mitwero, Manispaa ya Lindi, kati ya saa 10-11 alfajiri, baada ya kupigiwa simu kutoka kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wamezingira gari, linalodaiwa kutumika katika harakati hizo.

“Baada ya wananchi kulishuku lile gari walilifuatilia na kulizuia, na kupiga simu ofisini kwetu, ndipo nikaondoka mimi, vijana wangu na askari polisi kuelekea Mitwero,” alisema.

Alisema muda ulipofika, waliwakuta wananchi wamelizingira gari lenye namba za usajili T.563 BNA, na walipolipekuwa walifanikiwa kukuta mfuko uliokuwa na fedha taslimu Sh. milioni 4.2.

“Zile fedha tulizozikuta zilikuwa ni noti za Sh. 2,000 na Sh. 5,000,” alisema Chami.

Kamanda Chami alisema, Mikidadi alikamatwa Jimbo la Mchinga saa 5 usiku na kufikishwa kwenye Ofisi ya Takukuru kwa mahojiano.

Alisema Mikidadi anadaiwa kutoa Sh. 780,000 kujaribu kuwahonga maofisa wa Takukuru waliokuwa wanamhoji.

“Huyu mheshimiwa wakati akiendelea kuhojiwa aliwaomba awape Sh. 780,000 alizokuwa nazo ili yaishe,” alisema Chami.

Aliongeza kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa taratibu za ki-ofisi, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wao.

Watuhumiwa hao walipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kupitia simu zao za kiganjani ili kuzungumzia tuhuma hizo, simu zao zilizimwa.

Baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi wa CCM, walioshiriki kufuatilia nyendo za wagombea wao na hatimaye kufanikisha kukamatwa kwao, huku wakiomba majinayao yasiandikwe gazetini, wamewaambia waandishi kuwa, kukamatwa kwao hakuna lengo la kuwakomoa, bali ni kurejesha heshima ya chama kwa wananchi.

“Sisi ni miongoni mwa tulioshiriki kuanzia saa mbili usiku hadi alfajiri, na wakati tukiwa kwenye doria hiyo, tulipigiwa simu na raia wema kwamba kuna magari mawili, likiwemo Rav 4 rangi nyeupe ambaye ni mgombea ubunge hapa jimbo la Lindi mjini,” alisema mmoja wao.


Hili ni tukio la pili kwa wagombea ubunge kupitia CCM mkoani Lindi, kukamatwa na  Takukuru. Juzi Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alihojiwa na taasisi hiyo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top