Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

SIASA IMEPAMBA MOTO: Siri ya Slaa yafichuka

 
*Mbowe asema walitofautiana kuhusu Lowassa
*Asema chama hakitayumba kamwe, Mnyika aibuka
Emeresiana Athanas
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametoa siri ya kutoweka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa akisema kuwa walitofautiana naye wakati wa kujadili suala la ujio wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ndani ya chama hicho.
Kauli ya Mbowe imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Dk. Slaa kutoonekana katika matukio muhimu yanayohusu chama hicho, yakiwamo ya kumpokea Lowassa ambaye alihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni.
Lowassa ambaye aliwania urais kupitia CCM na baadaye jina lake kukatwa, alitangaza kuhamia Chadema Julai 28, mwaka huu, katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, akisema kuwa CCM siyo mama yake wala si baba yake ameondoka ndani ya chama hicho kwa sababu ya mizengwe.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Chadema, Mbowe alisema Dk. Slaa alikuwa akihudhuria vikao vyote vya Kamati Kuu vilivyokuwa vikijadili suala la Lowassa, lakini walitofautiana dakika za mwisho.
Mbowe alisema suala la Lowassa walilitafakari na kulichunguza kisayansi, lakini wakati wa majadiliano ya uamuzi wa mwisho ndipo tofauti zilipoanzia.
Alisema baada ya Dk. Slaa ambaye aligombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2010, kwenda tofauti na vikao yeye kama mwenyekiti alikaa na kuzungumza naye wakakubaliana kwamba chama kiendelee na mchakato wake na akiwa vizuri atajiunga kwa ajili ya kuendelea nao.
“Kamati Kuu ilikaa na kutafakari ujio wa ugeni mkubwa kwa kujadiliana na kuridhika pasipo shaka kwamba ujio wa Lowassa ni mipango ya Mungu katika kushirikina nasi na kuongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha tunashinda,” alisema.
Alitumia msemo wa kuwa ‘maji yana kupwa na kujaa’ hivyo chama hicho hakiwezi kumsubiri Dk. Slaa, Mbowe au Profesa Mwesiga Baregu na kwamba katika kuzungumza naye walikubaliana waendelee na safari ataungana nao.
“Najua kulikuwa na hofu ndani na nje ya chama kuhusu ukimya wa Dk. Slaa, hivyo niwatoe hofu tu na kuhusu taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ni uzushi tu, kwa sasa anapumzika kwa muda,” alisema Mbowe.
Alisema chama kitaendelea na safari yake, kwani hakiwezi kusubiri uamuzi wa mtu binafsi hususan katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi.
Mbowe alifafanua kuwa kauli aliyoitoa kwenye mkutano huo ni kwa niaba ya chama na si ya kwake, kwani ameamua kusema ukweli na kwamba chama kimekubaliana na uamuzi wa Dk. Slaa.
“Kwa hulka yake na tunajua anatupenda na sisi tunampenda, tunamwombea apate ujasiri wa kutambua sauti za wengi ni mipango ya Mungu, kwani katika chama chetu kitu kikipitishwa na mkutano wa chama hata kama si kwa asilimia 100 kitapitishwa,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema chama kitaendeleza mazungumzo naye, kwani wana imani chama kipo salama na kupasuka kwa sasa ni ndoto.
Alisema katika chama hicho hakuna siri bali kinaendeshwa kimikakati.
Mnyika
Akizungumzia kuhusu hofu iliyojengeka kwa kutoonekana kwa muda kwa Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, Mbowe alisema alikuwa anaumwa, lakini kwa sasa amerejea kufanya kazi za chama.
“Najua mlikuwa mkijiuliza kuhusu Mnyika, lakini alikuwa anaumwa na sasa amerudi na Tundu Lissu naye yupo hapa, pia mnaweza kushangaa hata Dk. Slaa kesho akaja,” alisema.
Ujio wa Lowassa
Kuhusu ujio wa Lowassa, alisema upepo wa siasa unabadilika, hivyo katika mazingira hayo chama hicho kimempata pamoja na baadhi ya wabunge na madiwani kutoka vyama vingine vya siasa kikiwemo na CCM.
“Hii ni fursa ya kuiondoa CCM na itaondoka, hivyo lazima tuweke mikakati ya kumpokea mwanachama wa chama chochote na tuko tayari kumpokea Mtanzania yeyote mwenye mawazo chanya na Serikali hata akitokea chama tawala,” alisema.
Mbowe alisema wao hawana rafiki wa kudumu, lakini wanataka malengo ya kudumu na kuiondoa CCM madarakani.
Alisema ujio huo umezua hofu kwenye kamati kuu ya chama, baraza kuu kwa wagombea ubunge na udiwani kuhisi kwamba wanaweza kuwapiku na kubainisha kuwa malengo ya chama ni mapana kuliko matamanio ya mtu.
“Hofu kuhusu watu wanaoingia Chadema ni minyukano ya kisiasa na tuna hakika tutashinda kwa kujenga maslahi mapana ya nchi,” alisema Mbowe.
Alisema kutokana na ujio wa Lowassa, wabunge na madiwani wengine ni pigo kwa CCM, kwani haijawahi kupata kipigo kubwa kama hilo na kwamba chama kinaendelea kuwasubiri wanachama wengine watakaoingia Chadema.
“Ujio huu ni pigo kubwa kwani kuondoka kwa Mrema (Agustine) CCM mwaka 1995 ni asilimia 25 ya pigo kama walivyolipata kwa kuondoka Lowassa,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alifafanua kuwa CCM ni chama kilichojaa rushwa na Chadema ina uadilifu na kwamba si chama cha kusafisha na kuwatakatisha wachafu, kwani kilichowaunganisha siyo dini wala kabila bali ni imani ya chama hicho.
Mbowe alisema chama hicho ni chama cha siasa kilicho makini na Mtanzania yeyote ana uhuru wa kujiunga. “Hiki ni chama cha watu kwani tungeamua kufunga milango yote na kukifanya chama cha viongozi mnadhani kingeimarika na kuwa namshikamano?” alihoji.
Alisema chama hicho katika miaka 25 kimejijenga na kwamba kuungana kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ni azma ya pamoja kwani vimekubali Chadema kuongoza pambano la kupambana na CCM.
“Sisi ni chama kaka mkubwa, kwani zoezi hili lililopo ni kubwa kuliko ukubwa wetu wa vyama vyetu CCM siyo rafiki, hivyo kwa namna Mungu alivyoamua kukilinda chama chetu wanachama wa chama tawalam wanahamia kwetu,” alisisitiza.
Mgombea urais
Mbowe alisema chama hicho leo kitampitisha na kumtangaza mgombea urais na mgombea mwenza atakayepeperusha bendera ya chama katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema kutakuwa na mapitio ya ilani ya uchaguzi itakayopendekezwa na kupitishwa.
“Huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo Ukawa tunalazimika kukaa vikao mara kwa mara kujadili mustakabali wa kupata wagombea wetu, hivyo vyama vinavyounda umoja huu umetupa heshima ya kumsimamisha mgombea urais mwaka huu,” alisema.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top