Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

KIMENUKA: RAIS KIKWETE AIJIA JUU NCAA WAKIONA CHAMOTO LEO



Rais Jakaya Kikwete, ameijia juu Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na menejimenti yake akiitaka kufanya utatifi zaidi kuhusu mambo ya kale katika hifadhi hiyo ili yaweze kuongeza mazao zaidi ya kuvuta watalii wengi badala ya wanyama na kreta pekee.

Akiweka jiwe la msingi jana la jengo la kitega uchumi la NCAA litakalokuwa na ghorofa 15  katikati ya Jiji la Arusha, Rais Kikwete alisema wakati nchi zingine kama Misri na Afrika Kusini zikiendelea na tafiti za mambo ya kale, wataalam wa Tanzania (Ngorongoro) wameacha kufanya utafiti.

Alisema kwa mfano utafiti wa nyayo za binadamu wa kwanza kama ulivyofanywa na Dk. Leakey, haujaendelea tena na hata uhifadhi wa nyayo hizo kama ulivyo sasa unahatarisha kupoteza ushahidi wa uvumbuzi huo.

“Ngorongoro haiwezi kuishinda Serengeti inapokuja suala la wanyama…watalii wengi wanapenda kupita Ngorongoro sio kuangalia wanyama bali vivutio kama kreta yenye wanyama, mchanga unaotembea na historia ya mambo ya kale,” alisema na kuongeza, “lazima akili ibadilike na kuongeza bidhaa zaidi ya wanyama.”

Hata hivyo, aliipongeza NCAA kwa kubuni kitega uchumi kwa kuamua kujenga jengo hilo litakalokuwa la ghorofa 15.

Alisema jengo hilo lililopewa jina la Jakaya Kikwete Ngorongoro Tower, litapendezesha taswira ya jiji la Arusha.

Mapema Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmood Mgimwa, alimpongeza Rais Kikwete kwa kufanya ziara za kikazi mara nyingi na zile za mapumziko katika Hifadhi ya Ngorongoro, jambo ambalo limekuza kwa kiasi kikubwa utalii wa ndani.

“Hivi sasa wananchi wengi nchini pamoja na familia zao wameanza kuhamasika kuja na kutembelea hifadhi hii ya kwa ajili ya kujiburudisha na kujifunza hifadhi ya mazingira, maisha na tabia mbalimbali za wanyamapori wanaopatikana katika Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema.

Akitoa taarifa kuhusu jengo hilo kwa Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Balozi Mwanaidi Maajar, alisema gharama za ujenzi wa jengo hilo hadi kukamilika kwake Novemba mwakani itakuwa zaidi ya Sh. bilioni 42.3.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top