Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

RAIS KIKWETE AMEKICHAFUA TENA ZANZIBAR, AMLIPUA MAALIM SEIF VIBAYA KAMA HAMJUI VILE



Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amemrushia vijembe Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad, kwamba hana hoja ya kudai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)haijafanya lolote kwa kuwa naye alikuwa ni sehemu ya serikali hiyo.
Rais Kikwete amesema takriban nusu ya Baraza la Mawaziri wa SMZ walitokana na Cuf, hivyo Maalim Seif hana sababu ya kutoa lawama kwamba SMZ haijafanya maendeleo yoyote Zanzibar.
"Si Makamu wa Kwanza wa Rais? Na kama aliona haridhishwi si angejiuzulu? alihoji Rais Kikwete alipokuwa akihutubia mkutano wa ufunguzi wa kampeni wa chama hicho visiwani Zanzibar jana na kuongeza kwamba hajawahi kuona umati mkubwa kiasi kile visiwani humo tangu awe madarakani.
Alisema wanaosema Zanzibar hakuna maendeleo, siyo kweli kwani maisha ya Wazanzibari sasa yamebadilika siyo kama miaka iliyopita.
Aidha, Rais Kikwete alishangazwa na umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza jana kwenye mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni katika viwanja vya Demokrasia visiwani humu jana.
 “Wallah sijawahi kuona watu wengi kiasi hiki kwenye uwanja huu.! Tumeshinda hatujashinda? Shein Rais au siyo Rais na  wengine ni wasindikizaji.” alisema na kuhoji Rais Kikwete.” 
Alisema kwa jinsi alivyouona umati huo mkubwa kiasi hicho, ni ishara tosha kuwa Dk. Shein tayari ameshashinda anachosubiri ni kuapishwa tu.
“Usione vyaelea ujue vimeundwa na muundani ni CCM, nchi ina amani, Zanzibar imetulia," alisema.
Rais Kikwete alisema uvumilivu na utulivu ni uongozi mzuri wa CCM na kwamba hata wanavyoongea kwenye majukwaa wanaonyesha siyo watulivu wala wavumilivu, hivyo wasipewe nafasi.
Akimwelezea mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohammed Shein, alisema ni mtu makini na siyo mpole ndiyo maana anafanya maamuzi magumu.
“Kama kuna kipindi Dk. Shein alipata wakati mgumu wa uongozi wake ni kutokana na usumbufu wa wapinzani,” alisema Rais Kikwete.
Aidha, Rais Kikwete alisema wapo viongozi walioingia madarakani, lakini hupata kigugumizi cha kutaja neno `Mapinduzi.'
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni wa tofauti kwa kulinganisha na miaka mingine na kuufananisha na mchezo wa mpira wa kukabana.
"Kama ni mpira mwaka huu, ni man to man. Tunatakiwa kuhakikisha tunakuwa makini na kuhakikisha chama kinapata ushindi kwa kupiga kura,” alisema.
Aliwataka wafanye kampeni za nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba na shuka kwa shuka mpaka wahakikishe Dk. Shein anaingia Ikulu.
Kuhusu kauli ya Malim Seif kuwa upinzani upewe siku 100  kuhakikisha wanashughulikia suala la haki ya Zanzibar kumiliki rasilimali zake za mafuta na gesi, Rais Kikwete alisema jambo hilo tayari ni ajenda ya serikali.
Alisema serikali ilijitahidi kutafuta wanasheia wawili ambao walipitisha sheria nzuri za umiliki wa mafuta na gesi baada ya Bunge kupinga suala hilo.
SHEIN KUENDELEA KULINDA MUUNGANO
Kwa upande wake, Dk. Shein alisema ataendelea kuulinda Muungano pamoja na kuyaenzi Mapinduzi pamoja na  kulinda sekta ya mafuta na gesi kwa maslahi ya Wazanzibar endapo akichaguliwa kwa mara ya pili kuingoza Zanzibar.
Kadhalika, amesema ataendelea kulinda amani iliyopo kwa kuwa bila amani, umoja na utulivu, maendeleo hayatapatikana.
Dk. Shein alisema katika miaka mitano aliyokuwa madarakani amedumisha Mapinduzi kwa kushirikiana na Marais waliomaliza muda wao wa uongozi wa Bara na Visiwani.
“ Tutaendeleza umoja uliokuwapo kati ya Wazanzibari na Bara kwa kuwa sote ni kitu kimoja na ni ndugu, hivyo hatuna sababu ya kubaguana,” alisema Dk. Shein.
Aidha, alisema hatamuogopa mtu yeyote katika kuhakikisha amani ya nchi haipotei kwa kusimamia haki na sheria kwa kila Mtanzania.
Pia alisema atakikisha anaitetea Tanzania katika medani ya kimataifa.
UCHUMI WA ZANZIBAR
Dk. Shein alisema uchumi wa Zanzibar umekua kutoka asilimia 5.2 mwaka 2010 na mwaka 2011 hadi asilimia 7.2 mwaka huu ikiwa ni juhudi za Serikali inayoongozwa na CCM.
MKAPA
Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alisema ana imani na Dk. Shein kwa kuwa amefanya naye kazi kwa muda mrefu na anamfahamu utendaji wake wa kazi kuwa ni muadilifu, mchapakazi na ni mtu anayewania maendeleo ya wananchi wote bila ubaguzi.
Alisema Zanzibar inatakiwa kuwa na viongozi watakaouenzi Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar pasipo kuwasahau waasisi na watu waliojitolea uhai kwa ajili ya taifa.
“ Ni fahari kwangu kuwa nina imani na Dk. Shein kuingoza tena Zanzibar kwa miaka mitano mingine ijayo kwa kuwa ataiweka Zanzibar katika mikono iliyo salama,” alisema Mkapa.
MWINYI
Naye Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema Wazanzibari wanapaswa kuchagua kiongozi mwenye maslahi na taifa lake na mwenye kuileta amani Zanzibar.
Alisema Dk. Shein ndiye kiongozi anayefaa kuiongoza Zanzibar kwa kuwa anajua Wazanzibar wanahitaji nini
KARUME
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alisema Zanzibar ina historia kubwa.
Alisema mwaka 1992, ilibadilishwa Katiba ya Zanzibar na ile ya Muungano na kuruhusu mfumo wa vyama vingi nchini.
Alisema amani inayodumu Zanzibar haikuja kwa uzi wa buibui kwa kutembea, bali ililetwa na Marais waliotangulia wa CCM.
Alisema wanzibar wanapaswa kulinda amani na kuwa nchi moja kama ilivyoachwa na marais hao waliotangulia.
DK. BILAL
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alisema uongozi wa nchi umekuwa ukiongozwa na CCM tangu ilipokabidhiwa kutoka kwa wakoloni.
"Bila ya uongozi wa CCM, nchi itakuwa matatani, bila ya uongozi wa CCM, amani itakuwa shakani na utulivu hautakuwApo pamoja na maendeleo hayatapatikana," alisema.
BALOZI SEIF ALI IDDI
Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Balozi Seif  Ali Iddi, alisema Dk. Shein amefanya mambo mengi ya maendeleo kwa kushirikiana na upinzani kwa miaka mitano iliyomalizika.
Alisema mwaka huu ni wa CCM kuishinda Cuf kwa kishindo na kwamba ni mwaka mwisho wa Cuf kushindana na CCM kiushindani.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top