Wakili wa Serikali, Salum Msemo na Wankyo Simon na Faraja Nchimbi, jana waliwataja washtakiwa hao kuwa ni Meneja wa Usalama wa TAA, Clement Mbaruck (46) na maofisa wake, Emmanuel Msanganiye (54), Salum Mnyones (33) na Albadri Mshana (31).
Wakili Msemo alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kuwa Julai 5, 2015 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) washtakiwa hao walikula njama ya kusafirisha nyara za Serikali kinyume na Kifungu cha 385 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyodanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alidai kuwa kati ya Julai 2 na 6, 2015 katika uwanja huo kwa makusudi waliendeleza michoro ya kihalifu kwa kuruhusu usafirishwaji wa kilogramu 150 za meno ya tembo, meno ya simba 21 na kucha za simba 35.
Wakili Msemo alidai kuwa Julai 5, 2015 washtakiwa hao walifanya hivyo bila ya kuwa na kibali cha usafirishaji kutoka kwa mkurugenzi wa wanyama pori .
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Julai 2 na 5, mwaka huu wakiwa waajiriwa wa TAA kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaidia kusafirisha nyara hizo wakati ni ukiukwaji wa Kifungu cha 82 (1) na 84(1) cha Sheria ya Wanyama Pori Sura namba 5 ya mwaka 2009.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hawakuruhusiwa kuzungumza chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na washtakiwa walipelekwa rumande.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 28 kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la



Post a Comment