Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi umesema mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad, anaupotosha umma juu ya mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais, Ali Mohamed Shein.
Aidha, umoja huo umesema kauli iliyotolewa na mgombea huyo wa urais kuwa atatoa ajira kwa vijana wote wa Zanzibar katika kipindi kifundi atakapochaguliwa kuwa Rais ni kuwarubuni na kuwadanganya wananchi ili wampigie kura.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UVCCM kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wake, Shaka Hamdu Shaka, Maalim Seif amekuwa akipotosha na kuudanganya umma kuwa serikali hiyo imeshindwa kufikia maendeleo yake tangu iundwe miaka mitano iliopita.
Shaka alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar huongwazwa kwa pamoja kati ya vyama vya CUF na CCM, hivyo madai anayotoa Maalim Seif yanalenga kutaka kupigiwa kura kuliko ukweli halisi.
Kwa mujibu wa Shaka, serikali hiyo imetekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo kama kukuza uchumi, kuboresha huduma za afya, miundombinu, utalii na elimu.
Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Shein pia imepandisha bei ya karafuu, zao ambalo ni tegemeo kubwa kiuchumi kwa Wazanzibari wengi.
Aidha, alisema chini ya uongozi wa Dk. Shein serikali hiyo imefanikiwa kupandisha mishahara kwa watumishi wa umma mara tatu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jambo ambalo alisema ni mafanikio makubwa katika kuimarisha huduma na maendeleo ya jamii.
CHANZO: NIPASHE


Post a Comment