Dar es Salaam. Wakati muda wa `mapumziko’ ya bomoabomoa ukimalizika leo huku jaribio la kupata zuio la muda likiwa limewekwa kiporo, wakazi wa Jangwani ambako nyumba zitaanza kubomolewa leo, jana waliweka mabango barabarani yanayotuma ujumbe wa aina mbalimbali kwa Rais John Magufuli.
Bomoabomoa hiyo ilianza Desemba mwaka jana likilenga nyumba zilizojengwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, lakini lilisitishwa kwa siku 14 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi hadi Januari 5, mwaka huu kuwapa nafasi wakazi kuondoka kwa hiari yao kuokoa mali zao.
Wakazi wa Jangwani walitumia mwanya huo wa kusitisha ubomoaji, kufungua kesi Mahakama ya Ardhi kupinga kuondolewa maeneo hayo bila ya kupatiwa sehemu nyingine na kuwasilisha ombi za zuio la ubomoaji, lakini chombo hicho cha sheria kilikataa kubariki mambo hayo ya kutaka sitisho la bomoabomoa liendelee wakati kesi ikiendelea mahakamani.
Wakati wawakilishi wa wakazi hao wakiwa mahakamani katikati ya jiji, watumishi wa halmashauri za jiji waliendelea kuweka alama nyumba zinazotakiwa kubomolewa wakiwa wamesindikizwa na ulinzi mkali wa polisi.
Hakukuwepo na wakazi waliojitokeza kuzuia uwekaji alama hiyo ya “X” inayotaarifu kuwapo kwa ubomoaji, lakini mabango ya maboksi yaliyosimikwa kwenye vifusi na maeneo mengine ya jangwani, yanatosha kuelezea hisia za wakazi hao wanaoishi maeneo ambayo yametangazwa kuwa hatarishi.
“Magufuli nafsi hizi zitakulilia hadi kiama,” linasema bango moja kati ya mengi yaliyosimikwa maeneo mbalimbali ya Jangwani jana.
“Magufuli mwambieni Said Meck Sadiki atuonyeshe viwanja vyetu,” linasomeka bango jingine likimaanisha Rais amwambie mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam awaonyeshe viwanja vyao.
Bango jingine liliekeleza lawama kwa Waziri Lukuvi.
“Nyumba unayolala, gari unalotumia wewe Lukuvi, mke na watoto wako ni kodi zetu acha udikteta,” linasema bango hilo.
Bango jingine liliandikosoa sera ya utoaji elimu bure, wakati baadhi ya wananchi hawana makazi.
“Elimu bure, kwa kulala hakuna,” liliandikwa bango hilo la boksi ambalo lilisimikwa juu ya kifusi.
Ulinzi mkali
Maofisa kadhaa waandamizi kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendelleo ya Makazi wakiwamo wahusika wa mipango miji jana waliendelea na shughuli hiyo ya kuweka alama ya ubomoaji katika maeneo ya Kigogo na Buguruni Sukita.
Vilio kutoka kwa baadhi ya wanawake katika maeneo hayo vilipasua anga wakati wakazi hao wakishuhudia nyumba wanazoishi zikiwekwa alama hiyo.
Afisa mazingira mwandamizi wa NEMC, Anrold Kisiraga alisema wanatekeleza hatua hiyo kwa maeneo hayo ni hatarishi kwa maisha ya binadamu hasa mvua zinazonyesha, lakini pia kunafanyika shughuli ambazo zinaharibu mazingira, ikiwamo uchimbaji wa mchanga.
“Kuna mito 11 jijini Dar es Salaam ambayo mabonde yake yamevamiwa, nasi tunatakiwa kuwaondoa watu hao kwa kubomoa makazi yao. Mito hiyo ni Kawe, Mlalakuwa, Mjigi, Nyakasangwe, Kiziga, Sinza, Mbezi, Mineva, Msimbazi, Mzinga na Tegeta,” alisema.
“Inatubidi NEMC tushirikiane na taasisi nyingine ambazo zinahusika, kwa kuwa pia wapo wengine ambao hutiririsha majitaka kwenye mifereji, hivyo kuhatarisha maisha,” alisema.
Katika baadhi ya maeneo watu kadhaa waliamua kuvunja nyumba zao wenyewe, waking’oa mabati, madirisha na milango, lakini wengine waliamua kuwasindikiza waliokuwa wakiweka alama kwa kuwaimbia nyimbo za kumsifu Rais Magufuli.
“Magufuli selema, selema selema, acha waisome namba ee Magufuli mbele kwa mbele amejipanga. Mwaka huu wataisoma,” waliimba watu hao wakichombezana wao kwa wao baada ya nyumba zao kuwekewa alama hiyo.
Mkazi mmoja wa eneo hilo, Kassim Ngulangwa (37) alisema ingawa wanaumia, ukweli unabaki kuwa ukweli kwamba mvua zinaponyesha hutawaliwa na mashaka kutokana na mafuriko yanayowakumba.
“Serikali ingeangalia jinsi ya kutusaidia kupata viwanja mahali pengine. Sisi ni wananchi wake, hii hatua kwa upande mmoja inatuumiza kwa sababu hatuna pa kwenda, lakini ni wazi kwamba tumekuwa tukiishi kwa mashaka wakati wa mvua,” alisema.
Wiki iliyopita , taharuki ilitanda kwenye maeneo ya Kigogo na barabara inayotoka makao makuu ya klabu ya Yanga hadi kona ya Kigogo Darajani baada ya vijana kuzifunga kwa muda kabla ya askari kufika na kupiga mabomu ya machozi zaidi ya 15 kujaribu kuwatawanya
Kortini leo
Wakati maofisa hao wakiendelea na uwekaji alama, wawakilishi wa wakazi hao walikuwa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kufuatilia kesi yao ya kupinga ubomoaji kutokana na kutopewa eneo mbadala.
Wawakilishi hao saba, Ali Kondo Mshindo na wenzake Sita wanaowakilisha wakazi 681, wameomba kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi kwenye kesi ya kupinga ubomoaji huo.
Maombi hayo ya kibali namba 822 ya mwaka 2015, yaliyofunguliwa dhidi ya Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) yalikuwa yasikilizwe jana na Jaji Panterine Kente, lakini haikuwezekana baada ya mawakili wa upande wa pili kuomba muda wa kuwasilisha hati ya kiapo.
Mawakili hao, Balton Mahenge wa Manispaa na Gabriel Malata anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu na Nemc, kwa nyakati tofauti waliieleza mahakama kuwa walipokea taarifa ya kufunguliwa kwa maombi hayo pamoja na hati za maombi Desemba 31, 2015.
Walisema kuwa kwa kuwa jana ilikuwa siku ya kwanza ya kazi na kwamba kulingana na asili ya kesi hiyo, wanaomba wapewe muda wa kuwasilisha hati kinzani ya kiapo ili waweze kuielezea mahakama vizuri.
Lakini wakili wa watoa maombi hayo, Abubakar Salim akaomba mahakama itoe amri kwa pande zote kudumisha hali ilivyo kwa sasa, kwa maana ya kazi ya bomoabomoa kuendelea kusitishwa na wakazi wa eneo hilo kuendelea kuishi hadi hapo itakapotoa uamuzi.
“Hatuna pingamizi kwa wajibu maombi ya kuleta hati ya kiapo kinzani, ila tunaomba mahakama yako tukufu itoe amri ya ku-maintain status quo (kudumisha hali ilivyo), katika kipindi hiki tunapojibizana kwa maandishi,” alisema Wakili Salim.
Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na upande wa wajibu maombi na hivyo kuibua mvutano wa kisheria, baada ya Malata kudai kuwa kwa sasa watoa maombi hao hawana hadhi ya kuwasilisha maombi ili mahakama itoe amri yoyote kwa kuwa hawatambuliki mahakamani.
Malata alisema maombi yaliyoko mahakamani sasa ni ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi na kwamba kwa kuwa maombi hayo hayajasikilizwa, hawana sifa ya kuwasilisha maombi ya amri hiyo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Kente aliamuru wajibu maombi wawasilishe mahakamani hati za viapo kinzani Januari 8, na atatoa uamuzi wa mambo hayo leo.
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Beatrice Moses na James Magai
Post a Comment