Ntungamo. Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amesema hawezi kuachia madaraka kwa sababu mazao yake yote aliyoyapanda ndiyo yanaanza kutoa matunda.
Akizungumza
kwenye mkutano wake wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini humo,
Museveni alisema akiachia madaraka kwa sasa atakuwa hajawatendea haki
raia wa Uganda.
“Wale wanaosema, ‘muache aende, muache
aende’ wanapaswa kufahamu kwamba huu siyo wakati wa kufanya hivyo,”
alisema Museveni wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika wilaya ya
Ntungamo
“Huyu mzee aliokoa nchi hii, mnaweza kumtaka
aondoke? Ninawezaje kuacha shamba la migomba ambayo nimeipanda mwenyewe
na limeshaanza kutoa matunda?” alihoji Museveni na kuongeza:
“Lazima tuzingatie maendeleo, wakati wangu utafika na nitaondoka.”
Wagombea saba watashiriki kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini humo Februari 18 mwaka huu ili kumuondoa Museveni madarakani.
Kiongozi
huyo aliyekaa madarakani tangu mwaka 1986, anachuana vikali na
wapinzani wake, Dk Kizza Besigye na Amama Mbabazi, aliyekuwa waziri
mkuu.Mbabazi alisema akishinda urais atapitisha kipengele cha muda wa
rais kukaa madarakani wa vipindi viwili.
“Wakati yeye
(Museveni) aliponiambia kwamba hangestaafu na kuniomba nimuunge aendelee
kuwania urais , nilisema hapana na sasa niko hapa,” alisema Mbabazi
kwenye mkutano wa kampeni nchini humo
“Katika siku100
za kwanza nikiwa rais, tutarejesha vipindi vya rais kukaa madarakani
katika katiba na tutafanya tuwezalo kuhakikisha kuwa katika miaka mitano
ya kwanza tutafanya juu chini kuandaa kizazi chenye umri mdogo ili
kitwae madaraka Uganda,” alisema Mbabazi.


Post a Comment