Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ameagiza wizara zote zinazohusika kukutana haraka iwezekanavyo na kujadili viwango vipya vya nauli vinavyoendana na hali halisi ya maisha ya wananchi. “… sasa nataka mamlaka zote zilizohusika wakutane na kuja na viwango vipya vya nauli kama huyu mwekezaji ameshindwa aseme, Serikali inaweza kuendesha mradi yenyewe,” alisisitiza Majaliwa.
Wizara na taasisi zilizoagizwa kukutana ni Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi); Wizara ya Ujenzi na ya Uchukuzi; Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na kampuni ya UDA-RT.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam muda mfupi baada ya kurejea akitokea Ruvuma, alikokamilisha ziara yake ya kikazi jana, alisema viwango hivyo vilivyopendekezwa na vinavyotarajiwa kujadiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) havifai na havikubaliki.
Alisema Novemba 25, mwaka jana alitembelea mradi huo wa DART na kumuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mtendaji Mkuu wa DART pamoja na Wakala wa Barabara (Tanroads) kupitia mfumo mzima wa uendeshaji wa mradi huo, lakini hadi leo hakuna mpango wowote wa biashara uliowasilishwa serikalini na UDA-RT.


Post a Comment