Hayo yalibainika jana baada ya Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, kueleza wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni mjini hapa.
Katika swali lake la nyongeza, Nkamia aliitaka serikali ikiri kuwa mashine hiyo ambayo inatumika Muhimbili ni ile ambayo imechukuliwa katika hospitali hiyo, badala ya kudai kuwa imenunuliwa mpya.
Kutokana na kubanwa huko, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, alikiri kuwa mashine ilitoka katika hospitali hiyo.
Hata hivyo, alisema si kweli kwamba iling’olewa baada ya kuwa imefungwa bali ilikuwa kwenye mchakato wa kufungwa.
“Ni kweli mashine hiyo ilikuwa ifungwe Dodoma katika hospitali ya Benjamin Mkapa lakini majengo yalikuwa hayajakamilika hivyo serikali ikaamua ipelekwe Muhimbili,” alisema.
Dk. Kigwangalla alisema serikali iko katika mchakato wa kununua mashine mpya kwa ajili ya kufunga hospitali ya Benjamini Mkapa na majengo ya kufunga mashine hiyo kwa sasa yanaelekea kukamilika.
Katika swali la msingi, Nkamia alihoji mpango wa serikali wa kununua mashine mpya ya CT-Scan kwa ajili ya hospitali ya Muhimbili.
Akijibu swali la msingi, Dk. Kigwangalla alisema serikali imefuatilia mwenendo wa huduma ya vipimo vya radiolojia inayotolewa Muhimbili na kubaini ina upungufu.
Alieleza upungufu huo ni kuharibika mara kwa mara kwa CT-Scan na kusababisha usumbufu kwa baadhi ya wagonjwa kutopata huduma ya kipimo hicho kwa wakati.



Post a Comment