Baadhi ya vijiji katika tarafa ya Idodi mkoani Iringa havina mawasiliano ya barabara baada ya mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini kusababisha maji kujaa na kuvunja kingo za mto Mapogoro na kuingia kwenye makazi na mashamba ya wananchi wa kijiji cha Mapogoro na pia kukata mawasiliano ya barabara inayounganisha vijiji hivyo.
ITV imefika katika eneo hilo na kushuhudia maji yaliyochukua mkondo mpya yakiendelea kufanya uharibifu wa mashamba pamoja na kutishia baadhi ya nyumba za wanakijiji wa kijiji cha Mapogoro katika tarafa ya Idodi huku jumla ya familia tatu zikiwa hazina makazi kutokana na maji hayo kuharibu nyumba zao.
Mmoja wa wahanga wa mafuriko hayo Bibi Yuditha Msigwelo amesema siku ya tukio hilo usiku wa tarehe 29 Januari majira ya saa nane usiku akiwa amelala nyumbani kwake alijikuta akiwa amezungukwa na maji ndipo alipojaribu kutafuta msaada.
Kukatika kwa barabara hiyo ambayo ndiyo njia kuu kuelekea hifadhi ya taifa ya Ruaha kumesababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa njia hiyo wakiwemo watalii wanaolazimika kutumia njia mbadala na kutokana na hali hiyo mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela amefika katika eneo hilo kujionea athali zilizojitokeza pamoja na juhudi zinazofanyika na wakala wa barabara nchini Tanroad mkoa wa Iringa waliopiga kambi katika eneo hilo.


Post a Comment