Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

Mwili wa Mtanzania uliokuwa umezuiliwa India wawasili

Ndugu na jamaa wa familia ya Machanga wakiwa
Dar es Salaam. Hatimaye mwili wa Mtanzania Abel Machanga (24) aliyefariki dunia akiwa katika matibabu India, umewasili nchini jana na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Amana jijini hapa kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho.
Mwili huo ulizuiliwa katika Hospitali ya Cambodia Asia, India kwa mwezi mzima baada ya familia ya kijana huyo aliyeaga dunia Desemba 31, mwaka jana kushindwa kulipa deni la Sh35 milioni zilizotumika kwa ajili ya matibabu.
Akizungumza jana katika Hospitali ya Amana ulipohifadhiwa mwili huo, Baba mzazi wa marehemu, Revocatus Machanga alisema mazishi ya kijana wake yatafanyika kesho huko Pugu baada ya madaktari kujiridhisha kuwa mwili uko kwenye hali nzuri.
Machanga alivishukuru vyombo mbalimbali vya habari kwa ushirikiano vilioutoa mpaka kupata msaada wa kusafirisha mwili wa mwanawe. Alisema amepokea msaada kutoka kwa watu mbalimbali baada ya kusoma na kutazama habari zake.
“Nimepokea pole kutoka kwa watu mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba. Ninashukuru sana kwa kunifariji wakati huu wa majonzi,” alisema.
Aliwashukuru Watanzania wote waliomsaidia kwa hali na mali katika kumuuguza mwanaye mpaka alipofariki dunia na kusaidia kusafirisha mwili wake kurudi nchini kwa ajili ya mazishi.
“Mwanangu alipata shida sana, tulianza kumuuguza kuanzia hospitali ya Taifa ya Muhimbili mpaka India. Huko tukaambiwa alikuwa na matatizo mengine kabisa tofauti na yale tuliyoambiwa Muhimbili,” alisema.
Hata hivyo, aliwashukuru madaktari wote waliojaribu kuokoa uhai wa mwanawe akisema yaliyotokea ni mipango ya Mungu.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top