Spika wa Bunge, Job Ndugai, (pichani) amesema takribani asilimia 70 ya wabunge wa Bunge la 11 ni wapya hali inayolilazimu Bunge kuwapa mafunzo yatakayowawezesha kupambana na changamoto watakazokutana nazo wakati wa kufanya kazi za kamati.
Ndugai alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifunga
mafunzo ya siku tano kwa wajumbe wote wa Kamati za Kudumu za Bunge
yaliyoanza Januari 8 mwaka huu.
Alisema mafunzo hayo yanaibua changamoto ambazo kamati inakumbana
nazo pamoja na kupata ufafanuzi wa masuala ya msingi kutoka katika
Wizara, Idara,Taasisi na Wakala wa Serikali ambazo watakuwa wadau katika
utekelezaji wa majukumu ya kamati.
“Natarajia mafunzo haya yatatumika kama nyenzo muhimu katika
utendaji kazi wa siku hadi siku katika kamati zenu hasa ikizingatiwa
kuwa idadi ya wabunge wengi kwenye bunge hili ni wapya,” alisema.
Alisema kuhusu mafunzo ya jinsi ya kufanya tathmini namna ya
ufuatiliaji na utekelezaji wa bajeti, yatawapa uelewa wabunge wa masuala
yanayohusu uchambuzi wa bajeti na mipango ya Serikali.
Ndugai alisema mpaka kumalizika kwa mafunzo hayo ya wabunge wa
Bunge la 11 watakuwa na ujuzi wa msingi wa kuchambua masuala ya bajeti
na mipango ya Serikali.
Alisema mipango pamoja na bajeti ya Serikali ina uhusiano wa moja
kwa moja na wananchi katika majimbo wanakotoka wabunge na kwamba
wanatarajia kuwa wananchi watanufaika na Bunge katika vikao vijavyo
kutokana na weledi walioupata.
Katika mkutano huo wa mwisho wabunge walipata fursa ya kujifunza na
kujadili kuhusu bajeti ya serikali na mpango wa maendeleo wa miaka
mitano.
CHANZO:
NIPASHE


Post a Comment