Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhika na kiwango cha ujenzi wa daraja la Kigamboni lililokamilika kwa asilimia 99.9 ambalo linatarajia kukabidhiwa rasmi Aprili 17 mwaka huu baada ya kutumia zaidi ya shilingi bilioni 46 pamoja na dola za Kimarekani milioni 86.
Akizungumza kamati hiyo ilipotembelea daraja hilo mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mh.Norman Sigara licha ya kusisitiza daraja hilo limebadilisha mandhari ya Dar es Salaam amesema mkataba uliotumika ulikuwa mzuri kwa pande zote mbili jambo lililochangia fedha zilizotumika kutoongezeka kwa kiwango kikubwa.
Kufuatia kukamilika kwa daraja hilo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wameonyesha kuwa na wasiwasi kuhusu mfumo utakaotumika kupita kwa magari makubwa pamoja na kiwango cha tozo zitakazotumika ili kuwezesha daraja hilo kuwa suluhisho la kero ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo mengine.
Aidha baadhi ya wajumbe wameonyesha kuwa na wasiwasi wa kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa daraja hilo baada ya Mkandarasi kulipwa asilimia 80 tu ya fedha mpaka sasa huku thamani ya kiwango cha dola kwa sasa kikiwa kimeongezeka na kufikia shilingi elfu 2 wakati mkataba huo ulisaiiniwa kwa kiwango cha dola moja sawa na shilingi elfu moja na miatano 90.


Post a Comment