Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Askari waliopo kwenye operesheni inayofanywa Wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani zinaeleza kuwa baadhi ya watuhumiwa wamesema kwamba wanavamia vituo vya polisi ili kukusanya silaha ambazo zitawapa nguvu ya kugeuza utawala nchini ili uwe wa itikadi ya dini yao na wanavamia Vituo hivyo kwa ajili ya kuongeza idadi ya silaha katika himaya yao.
Gazeti la Jambo Leo limeandika kuwa watu hao wana mtandao nchi nzima na kwamba kutokana na imani yao ni ngumu kuwabadilisha msimamo wao hata wanapokuwa mbele ya vyombo vya dola.
Mwanajeshi mmoja ambaye aliongea na mwandishi wa habari wa Gazeti hilo alisema operesheni kama hizo amezifanya mara nyingi na hivi karibuni waliwakamata watuhumiwa wengine kama hao Morogoro nao walisema lengo lao ni kutaka kubadilisha utawala uwe wa itikadi ya imani ya dini yao.
Mtuhumiwa mmoja alipoulizwa kwa utani kwa nini hawaendi kuvamia maghala ya silaha Jeshini kama kweli wanataka kusimika serikali yao, alisema wameanza kukusanya silaha kwa vile ni wachache na kingine kinachowakwamisha ni jinsi ya kuingiza silaha ndiyo maana wanakusanya bunduki za ndani.
Uchunguzi unaonesha baadhi ya vijana wanatuhumiwa kuwa ndani ya mtandao huo na huwa wanatumiwa bila ya wao kuelewa undani jambo linalofanyika ili kuepuka siri kuvuja.



Post a Comment