Kiungo wa FC Platinum ya Zimbabwe, Thabani Kamusoko (kushoto) akiwa na meneja wa Yanga, Hafidh Saleh aliyempokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, jana.Picha na Khatimu
Dar es Salaam. Kiungo wa FC Platinum ya Zimbabwe, Thabani Kamusoko amewasili nchini kukamilisha uhamisho wake kujiunga na Yanga na kusema hakuja Tanzania kukalia benchi.
Akizungumza mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jana mchana, Kamusoko alisema anatambua anakuja kujiunga na Yanga ambao ni mabingwa wenye kikosi kinachoundwa na wachezaji nyota, na yuko tayari kugombea nafasi na mchezaji yeyote atakayemkuta.
Kamusoko alisema amefurahi kukamilisha safari yake ya kutua Yanga, lakini hana shaka na uwezo wake katika kuzitumikia nafasi mbili za kiungo mkabaji na hata kiungo mchezeshaji kutafuta nafasi ya kudumu katika kikosi hicho.
Alisema anatambua viongozi, mashabiki na hata wachezaji wenzake wana matarajio makubwa kwake, endapo kila kitu kitakamilika Yanga haitajuta kumsajili.
“Najua ubora wangu nipo tayari kocha akinipa jukumu lolote nafasi ya kiungo, lakini napenda kucheza kama kiungo mchezeshaji, najua maeneo hayo yote yatakuwa na watu nitakaowakuta hapa nitapambana,” alisema Kamusoko.
“Namuheshimu Niyonzima (Haruna) ni mchezaji mzuri nimekuwa na bahati nzuri ya kukutana naye mara kwa mara na sasa ni katika timu moja najua kuna wengine pia nitakutana nao hapa nafikiri kocha ataamua nani ampange katika timu yake.”
Pluijm kutobadili falsafa yake
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amesema hana mpango wa kubadili falsafa yake ya soka la pasi na kushambulia licha ya timu hiyo kutofanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika Jumapili.
Pluijm alisema falsafa ya soka la kushambulia ni nzuri na tayari imeshazoeleka na wachezaji wake, hivyo haoni sababu ya kuibadilisha bali atarekebisha upungufu uliojionyesha kwa nyota wa kikosi chake.
“Nitaendelea kutumia mfumo na staili hii ya uchezaji kwa timu yangu kwa sababu bado sijaona kama ina matatizo kwa wachezaji wangu. Kwa sasa hatuangalii yaliyopita, akili yetu tumeelekeza kwenye mechi zinazofuata ambazo lengo letu ni kushinda,” alisema.
Katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Pluijm na benchi la ufundi la Yanga wameonekana kuwa makini na kutilia msisitizo mazoezi ya kupiga pasi fupi fupi pamoja na kushambulia kitimu, jambo linaloonyesha kuwa wanataka kuona timu hiyo inatengeneza nafasi na kufunga mabao mengi.
Kuhusu mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, Pluijm alisema naamini timu yake itaibuka na ushindi, ingawa anajua watakutana na timu nzuri ambayo imetoka kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame.
Katika hatua nyingine, Pluijm amewatetea wachezaji wake wanaocheza safu ya ulinzi kwa kusema wanafanya kazi nzuri na hataki kuona watu wakiwalaumu iwapopindi timu hiyo isipopata matokeo mazuri.
“Nashangaa kuona watu wakitoa lawama kwa mabeki timu inapopoteza mchezo. Sikia, soka ni mchezo wa makosa na hakuna binadamu aliyekamilika” alisema. Aliongeza kuwa Yanga inaundwa na wachezaji bora na wenye vipaji


Post a Comment