Loading...
http://go.ad2up.com/afu.php?id=778977

UKAWA WANATAKA.Sheria itungwe kuruhusu muungano wa vyama

Viongozi  wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
Viongozi  wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)kutoka kushoto ni James Mbatia,akifuatiwa na Freeman Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba. 
Juzi vyama vya upinzani vimeandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya vyama vinne vya upinzani vinavyounda Ukawa, kumtangaza mgombea mmoja wa urais wa Jamhuri ya Muungano na mgombea mmoja kwa nafasi ya urais wa Zanzibar.
Tukio hilo lilifanywa kwenye Mkutano Mkuu wa Chadema uliofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD na wahudhuriaji wengi walionyesha shauku ya kuwepo muungano wa vyama vya siasa.
Shauku hiyo pia iliwahi kuonyeshwa na Msajili wa Vyama vya Siasa aliyestaafu, John Tendwa ambaye kabla ya kuondoka aliandaa muswada wa mabadiliko ya sheria namba 5 iliyoanzisha mfumo wa vyama vingi, ili kuruhusu vyama vya upinzani kuungana.
Tuna ushahidi wa nchi jirani ya Kenya ambako ushirika wa vyama vya upinzani ulianza kabla ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge wa mwaka 2002, ambapo vyama vya Democratic Party cha Mwai Kibaki, Ford-Kenya cha Michael Wamalwa na NPK cha Charity Ngilu na kuitwa National Alliance Party of Kenya (NAK).
NAK iliungwa mkono na vigogo waliojitoa chama tawala cha Kanu, ambao walianzisha chama cha siasa cha National Rainbow Coalition (NARC) na kushika madaraka na Mwai Kibaki kuwa rais wa kwanza kutoka upinzani tangu uhuru wa nchi hiyo.
Kwa kilichotokea juzi nchini kimedhihirisha shauku ya kuwapo sheria inayoruhusu muungano wa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi mkuu, hitaji hilo limeonekana wazi kwa namna Ukawa walivyopata tabu ya kupata mgombea mwenza, ambapo mwanachama wa CUF alilazimika kukihahama chama chake na kuingia Chadema, kwa lengo la kutimiza ndoto yao ya kuwa na ushirikiano.
Tunaamini kama Tanzania ingekuwa na sheria inayoruhusu vyama vya siasa kuungana wakati wa uchaguzi, ni imani yetu kwamba hata chama tawala chenyewe kingeweza kuwa na muungano wake na vyama rafiki.
Ni hoja finyu kudhani kuwa sheria hiyo ni kwa manufaa ya vyama vya upinzani pekee, kwani inawezekana chama tawala kikashinda nafasi ya urais, lakini kikashindwa kupata wabunge wengi ambao wangekiwezesha kumpata waziri mkuu. Lakini kama sheria ya kuunganisha vyama ipo, kinaweza kujenga ushirikiano na chama rafiki na kumpata waziri mkuu wanayemtaka.
Mfano kama huo uliwahi kutokea Uingereza wakati fulani, ambapo chama cha Conservative cha David Cameron ushindi wake haukukiwezesha kuunda serikali na hivyo kikalazimika kushirikiana na chama rafiki cha Liberal Democrat cha Nick Clegg. Cameron alikuwa Waziri Mkuu na Clegg kuwa Naibu Waziri Mkuu.
Kwa mantiki hiyo sheria ya kuruhusu muungano wa vyama vya siasa ina faida kwa pande zote, chama kilicho madarakani na upande wa vyama vya upinzani, kwani si lazima vyama vya upinzani kuungana vyenyewe, vinaweza kuungana hata na chama tawala kwa lengo la kuunda serikali ya pamoja.
Ni rai yetu muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ulioachwa na John Tendwa ufanyiwe kazi na msajili wa sasa wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi. Kama Tendwa ameacha kumbukumbu hiyo ni vema mrithi wake Jaji Mutungi akahitimisha kwa kuwezesha kuwepo kwa sheria hiyo ambayo ni manufaa pia kwa Watanzania na demokrasia kwa ujumla.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright JAMIIYETU | Designed By BAKI NASI
Back To Top