Polisi mkoa wa Ruvuma inamshikilia Januari Ponera (53), mkazi wa kijiji cha Naikesi, wilayani Namtumbo, kwa tuhuma za kukutwa na nyama ya tembo inayokadiriwa kuwa na kilo 13 aliyokuwa akiisafirisha kutoka Naikesi kwenda Songea kuiuza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5 asubuhi mtaa wa Mitawa, Manispaa ya Songea.
Alisema siku ya tukio askari wakiwa kwenye doria walimkamata Ponera akiwa na nyama hiyo aliyokuwa ameiweka kwenye kiroba akiisafirisha ndani ya basi la Kangaulaya ambalo lilikuwa linatoka kijiji cha Naikesi kwenda Songea.
Alisema askari polisi walipomkamata akiwa na mzigo huo, alisema alikuwa ameagizwa na mtu aupeleke Songea jambo ambalo walilitilia shaka na kuanza kumpekua na kugundua kuwa ni nyama ya tembo.
Kamanda Msikhela alisema thamani ya nyama hiyo haijafahamika na mtuhumiwa anashikiliwa na polisi wakati taratibu za kisheria zinafanyika ili kumpeleka mahakamani.



Post a Comment